Yanga yamtambulisha Litombo

Beki mpya wa Yanga, Yannick Litombo

KLABU ya Yanga jana ilitarajia kumtambulisha rasmi beki wake mpya, Yannick Litombo baada ya mchezaji huyo kukamilisha taratibu zote za kujiunga na miamba hiyo ya soka Tanzania Bara.

Yanga ipo nchini Morocco katika jiji Marrakesh ambako imeweka kambi ikijifua kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na tayari ratiba imetoka wamepangwa kuanza na Rivers United ya Nigeria.

Akizungumza kupitia Azam TV  Online jana, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano wa Yanga, Hersi Said  alisema beki huyo tayari amesharipoti kambini nchini humo na walitarajia kumtambulisha muda wowote jana.

Advertisement

“Tulishamalizana kila kitu na Litombo kilichobaki ni kumtambulisha kama ilivyokuwa kwa wachezaji wengine, yeye hakuja Dar es Salaam aliungana na timu huku Morocco sababu kuna baadhi ya vitu alikuwa anakamilisha kwenye klabu yake aliyokuwa akiichezea ya FAR Rabat,” alisema Hersi.

Kiongozi huyo pia alisema leo wanatarajia kumpokea kiungo wao Mganda, Khalid Aucho ambaye bado alikuwa hajaungana na wenzake kwenye maandalizi yao na baada ya kuwasili ataendelea na programu za timu ambazo zinaongozwa na kocha wao, Nasriddine Nabi.

Kiongozi huyo alisema mpaka sasa maandalizi yao yanaendelea vyema nchini Morocco na kocha wao Nabi ameridhishwa na kambi hiyo ambayo amesema itamsaidia kukiandaa kikamilifu kikosi hicho kwa ajili ya kufanya vizuri msimu ujao.

Aidha, Hersi alisema jezi ambazo zinatumiwa na timu yao kwenye mazoezi huko Morocco ni kwa ajili ya kambi hiyo tu na siyo jezi rasmi ya msimu mpya na kwamba utambulisho wa jezi mpya watakazozitumia msimu ujao utafanyika kwa kufuata utaratibu ambao wamekuwa wakiutumia misimu iliyopita.

Kabla ya kutua FAR Rabat, beki huyo kisiki alikuwa akiichezea AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambako aling’ara kabla ya kuonwa na Waarabu hao.