Yanga yapaa ubora Afrika
MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga wameendelea kung’ara baada ya kupanda kutoka nafasi ya 19 mpaka ya tisa kama moja ya timu inayofuatiliwa zaidi Afrika huku wapinzani wao wakubwa Simba wakishuka kwa nafasi moja kutoka ya tisa mpaka ya 10.
Yanga msimu huu imekuwa ikifanya vizuri kwenye ngazi ya klabu Afrika ambapo iko kwenye hatua ya nusu fainali Kombe la Shirikisho la Afrika na iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini.
Huku wapinzani wao Simba wakitolewa kwenye hatua ya robo fainali kwa mikwaju ya penalti na Wydad Casablanca ya Morocco.
Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za mpira wa Miguu lenye makao makuu yake Uswisi (IFFHS) limetoa orodha hiyo Mei Mosi, 2022 hadi Aprili 30, 2023 ambapo timu mbili kutoka Tanzania za Yanga na Simba zimeingia kwenye 10 bora.
Katika orodha hiyo, Al Ahly ya Misri wanaongoza wakiwa na pointi 228, nafasi ya pili ni Wydad Casablanca yenye pointi 172, Zamalek wanashika namba tatu wakiwa na pointi 155.
5, namba nne ni Pyramids wenye pointi 147 huku Far Rabat yenye pointi 128 inashika nafasi ya tano.
Miamba ya Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns wako namba sita wakiwa na pointi 127, Future FC inashika nafasi ya saba ikiwa na pointi 124.
2, namba nane inashikwa na Al Hilal Omdurman ya Sudan wenye pointi 123.4, Yanga ya Tanzania nafasi ya tisa pointi 118.5 na Simba inakamilisha 10 bora ikiwa na pointi 117.
Misri imeingiza timu nne na Tanzania na Morocco zimetoa timu mbili kila mmoja kwenye orodha hiyo na Afrika Kusini na Sudan zikitoa timu moja moja.