Yanga yatinga kibabe makundi CAFCL
DAR ES SALAAM: Baada ya kusubiri kwa kipindi cha miaka 25 hatimae Yanga wamefanikiwa kutinga hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika (CAFCL).
Mara ya mwisho kwa wababe hao wa kandanda la Tanzania kucheza hatua ya makundi ilikuwa ni mwaka 1998 na sasa rasmi wamevunja mwiko huo na watacheza hatua hiyo msimu huu.
Safari ya Yanga hadi wanafika hatua ya makundi, katika mchezo wa hatua ya awali waliiondosha Asas Djibouti kwa jumla ya mabao 7-1 wakishinda 2-0 ugenini na kisha 5-1 katika mchezo wa mkondo wa pili wakiwa nyumbani.
Hatua iliyofuata walipangwa kuminyana na miamba kutoka Sudan Almerrikh na wamefanikiwa kuwaondosha katika michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya Vilabu barani Afrika.
Mpaka wanatinga hatua ya makundi Yanga wamefunga jumla ya mabao 10 na kuruhusu kufungwa bao moja pekee.
Yanga wameiondosha Almerrikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-0 baada ya ushindi wa bao 1-0 katika mchezo uliopigwa leo katika dimba la Azam Complex Chamazi bao lilofungwa na mshambuliaji Clement Mzize kwenye kipindi cha pili cha mchezo huo.