YST yachagua 12 Lindi kushiriki maonesho Dar

TAASISI ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania (YST), imechagua wanafunzi 12 kutoka katika shule za sekondari sita za mkoa wa Lindi kushiriki maonesho ya kitaifa ya kazi za sayansi na teknolojia yatakayofanyika Desemba mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Wanafunzi hao walichaguliwa katika maonesho ya kimkoa yaliyofanyika Wilaya ya Lindi, ambapo shule 25 za mkoa huo zikiwa na wanafunzi 50 zilishiriki kuonesha kazi za sayansi na teknolojia walizozifanyia kwa muda wa miezi mitano.

Mwanzilishi Mwenza wa YST, Dk Gozibert Kamugisha amesema maonesho ya kitaifa yatafanyika Desemba 8 mwaka huu, ambapo yatashindanisha kazi bora za wanasayansi chipukizi  kutoka shule za sekondari mikoa yote ya Tanzania.

Amesema wanafunzi waliochaguliwa Mkoa wa Lindi, wamejaribu kugundua njia mbalimbali za kutatua matatizo ambayo jamii inakabiliana nayo kwenye masuala ya kilimo, afya, mazingira na kuweza kupata utatuzi wa masuala hayo.

“Vijana wetu wamejaribu kugundua njia mbalimbali za kuweza kutatua matatizo ambayo yanawakabili kwenye jamii zao hususani masuala ya kilimo, afya na mazingira na kuweza kupata utatuzi wa masuala hayo,” amesema.

Amesema maonesho ya kimkoa ambayo yameanza katika Mkoa wa Lindi, yatafanyika mikoa yote nchini Tanzania kwa lengo la kuchagua wanasayansi bora watakaoshiriki kwenye maonesho ya kitaifa ifikapo Desemba 8 mwaka huu.

Maonesho ya mwaka huu ya kimkoa yanalifanyika mkoani Lindi yamefanyika chini ya udhamini wa Taasisi ya Shell Tanzania, ambao wamefanikisha maonesho haya kwa asilimia kubwa.

Jumla ya tafiti bora 6 za kisayansi, zilichaguliwa kutoka kwenye maonesho hayo ambazo zitashiriki kwenye maonesho ya kitaifa yanayotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Dk Bora Haule, amelipongeza shirika hilo kwa kuwa mstari wa mbele kuwawezesha wanafunzi na waalimu kuwa wabunifu na wanasayansi wa siku zijazo.

Pia amewataka wanafunzi walioshiriki kwenye maonesho hayo kuongeza bidii kwenye tafiti zao kwa kuwa njia waliochagua ni njia sahihi na yenye manufaa kwao, kwa kuwa sayansi na teknolojia ni njia sahihi ya kutatua changamoto mbalimbali kwenye kijamii.

“Niwatie moyo sana vijana kwa hatua mliyoifikia ya kubuni miradi hii ambayo inasaidia kuleta suluhu kwenye jamii yenu, endelezeni tafiti hizi kwa manufaa ya baadae,” ameeleza.

Mratibu wa YST Mkoa wa Lindi, Ashura Lema amewapongeza wanafunzi kwa kuonesha ubunifu wa hali ya juu, ambao unatoa majibu dhidi ya changamoto zilizopo.

Amewataka wanafunzi hao kuendeleza vipaji na ubunifu waliouanza ili kuiwezesha jamii kunufaika na ubunifu wao.

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x