ZAIDI wa wakazi 1000 wa Mtaa ya Mihama, Kata ya Kitangiri iliyopo Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, wanatarajia kunufaika na mradi wa Zahanati ya Mihama inayotarajiwa kukamilika Juni 30 mwaka huu.
Hayo yamesemwa leo na mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Wilaya ya Ilemela Leonard Robert wakati wa ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya TASAF katika Wilaya ya Ilemela.
Akielezea zaidi kuhusu mradi huo, Robert amesema zahanati hiyo mpaka sasa imefikia asilimia 98 ya utekelezaji wake.
Amesema kwa sasa imebakia sehemu ndogo kukamilika, ambapo wanaendelea na utengenezaji wa sehemu ya kutupia takataka na kuiomba jamii ya mtaa wa Mihama na mitaa ya jirani kuhakikisha wanatunza mradi huo.
Amesema mradi huo mpaka kukamilika utagharimu Sh milioni 187 na kwamba katika Manispaa ya Ilemela wanayo miradi 21 ya TASAF na miradi hiyo ina gharama ya Sh bilioni 1.3.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mihama,Jonathan Shiwanda amesema zahanati hiyo ikikamilika itawasaidia kupata huduma ya afya.
Amesema kwa sasa wanatumia Zahanati ya Kirumba na Hospitali ya Sekou Toure, ili kupata huduma ya afya.