Zahanati yakabiliwa na uhaba wa wauguzi

ZAHANATI ya Shanwe inayohudumia zaidi wananchi 22,000 wa Kata ya Shanwe Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi inakabiliwa na uhaba wa wauguzi na kupelekea msongamano wa wagonjwa wanapokwenda kupata huduma.

Hayo yamebainika Februari 9,2024 wakati wa maadhimisho ya miaka 47 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo Diwani wa Kata hiyo Fadhili Makolokolo aliambatana na baadhi ya watendaji wa Chama hicho na Serikali kuadhimisha kwa kufanya usafi eneo la Zahanati ya Shanwe pamoja na kusikiliza kero za wananchi.

Akisikiliza kero hizo diwani Makolokolo amebaini changamoto ya upungufu wa wauguzi kutokana na uwepo wa muuguzi mmoja katika zahanati hiyo pamoja na changamoto ya maji kukatika mara kwa mara.

“Moja kati ya kero ambayo tumeikuta hapa ni pamoja na uchache wa wahudumu hususani kwenye kliniki, lakini daktari hakuna kwa hiyo tumewasiliana na DMO (Mganga Mkuu wa Wilaya) kaahidi kuwa kufikia kesho asubuhi atakuwa amelifanyia kazi na huduma itaendelea”

“Changamoto ni kubwa na hasa ukiangalia population ya watu wanaokuja ni wengi, ukiangalia wakinamama waliokuja hapa ni zaidi ya 300 kwa siku ya leo, utaona kuhudumiwa na mtu mmoja ni tatizo kwa hiyo tumemtaka DMO aje aone ukubwa wa tatizo na aweze kulitatua” amesema Diwani Makolokolo

“Kilichotokea hapa mganga mfawidhi hospitali hii amepatwa na shida ya tumbo na kufanyiwa operation (upasuaji) ya utumbo kwa hiyo yupo likizo ya magonjwa, na yule mwingine ambaye amekaimu kapata likizo.Hatukuwa na taarifa kabla lakini baada ya kubaini changamoto hiyo tuliwasiliana na DMO na ametuahidi kutuletea wauguzi” ameongeza.

Aidha kuhusiana na changamoto ya huduma ya maji kutotoka bombani kila siku diwani Makolokolo amesema tayari wamewasiliana na watu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mpanda (MUWASA) ambapo wameahidi kuwa watahakikisha wanatatua changamoto hiyo hasa kwa kipindi hiki ambacho miundombinu mingi ya maji na barabara imekatika na kupelekea mabomba mengi kupasuka.

Kwa upande wao wananchi wa Kata ya Shanwe wamefurahia na kuunga mkono jitihada za diwani huyo na baadhi yao kujitokeza katika zoezi hilo la usafi katika eneo hilo.

“Tuliona maadhimisho yetu tuyafanye Zahanati ya Shanwe kwa ajili ya kufanya usafi kwa kufyeka,kulima,kuziba na kuchimba mitaro ili kuhamisha maji yanayotoka kwenye dimbwi kuja kwenye Zahanati ili kudhibiti uharibifu wa miundombinu” amesema Hamad Mkandawile Mwenyekiti CCM Shanwe

Hata hivyo wananchi wa Shanwe wamepongeza hatua hiyo na kuiomba Serikali kutatua changamoto ya upatikanaji wa dawa kwa wakati pamoja na kutatua kero walizowasilisha kwa haraka.

Habari Zifananazo

Back to top button