KOCHA Mkuu wa Polisi Tanzania, Mwinyi Zahera amesema sare waliyopata kwenye mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union imewapa matumaini ya kushinda mchezo wa keshokutwa dhidi ya Ruvu Shooting.
Kocha huyo ameeleza kuwa hiyo ni kutokana na wachezaji wake kushika vyema mbinu na maelekezo anayowapa kwenye uwanja wa mazoezi.
“Tunacheza na Ruvu Shooting ni timu nzuri licha ya kutokuwa na matokeo mazuri, lakini Polisi hii siyo ile ya siku za nyuma, timu imeimarika kwa kiasi kikubwa naamini mwaka mpya tutauanza vizuri na watu watashangaa kuiona matokeo yakibadilika na kupanda nafasi za juu,” alisema Zahera.
Kocha huyo leo Desemba 31 ameeleza kuwa pamoja na timu yake kuwa nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi, lakini hawajakata tama wataendelea kupambana hadi mchezo wa mwisho na hiyo ni kutokana na mikakati waliyokuwa nayo ya kukiimarisha kikosi chao kupitia dirisha hili dogo la usajili msimu huu.
Polisi Tanzania imeshinda michezo miwili pekee na kupoteza michezo 12 na kwenda sare michezo mine, kitu ambacho kinawafanya kubaki nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 10.
Comments are closed.