DAR ES SALAAM: KAYA zaidi ya 200 katika mtaa wa Msimbazi Bondeni, Kata ya Jangwani, Ilala, Dar es Salaam zimelipwa fidia zihame kupisha mradi wa uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi.
Hayo yamefahamika ikiwa ni wiki moja tangu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa alipozungumza na wakazi wa kata hiyo Novemba 15 mwaka huu na kuwaahidi kuwa wangeanza kulipwa Novemba 16 mwaka huu.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Justin Bruno alisema hadi Novemba 19 kaya 200 zilikuwa zimeshalipwa fidia na bado kazi nyingine zinaendelea kulipwa.
Kwa mujibu wa Mchengerwa alisema zaidi ya asilimia 92 ya wakazi hao wameshahakikiwa tayari kwa kulipwa fidia.
Alisema fidia inayolipwa ni ya tathmini ya majengo na ardhi ingawa hawakustahili kulipwa fidia ya ardhi kwa kuwa walijenga kwenye maeneo hatarishi yasiyoruhusiwa kuwa na makazi.
Bruno alisema wanatarajia kuona wakazi hao wanaanza kuondoka kwa kuwa serikali imewapatia fedha watafute maeneo ya kwenda.
“Wapo ambao wameshalipwa lakini bado hawajaondoka, wamepewa mwezi mmoja na wiki mbili baada ya kupokea fidia zao wawe wameondoka, tunatarajia kila mmoja ataondoka ndani ya muda waliopewa,” alisema.
Mwaka 2022 Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia zilihitimisha mchakato wa kujadiliana kuhusu namna ya kupata fedha za utekelezaji wa mradi wa uendelezaji wa eneo hilo.
Zaidi ya dola 260 ziliidhinishwa na Benki ya Dunia ukiwa ni mkopo nafuu kwa kwa ajili ya utekelezaji wa lengo hilo.
Lengo la serikali kufanya maboresho katika eneo ya Bonde la Mto Msimbazi ni pamoja na kutafuta suluhu ya kudumu ya mafuriko katika Bonde la Msimbazi.
Mchakato wa kuboresha eneo hilo ulianza mwaka 2017 ukisimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais. Miongoni mwa miradi inayotarajiwa kutekelezwa ni bustani ya jiji, maduka makubwa, sehemu za kupumzika, kumbi za starehe na hoteli.
Comments are closed.