DAR ES SALAAM: SERIKALI imeendelea kufunga mitambo ya kisasa zaidi ikiwemo mitambo ya mawasiliano kwa njia ya sauti VHF yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 35 inayotoa uhakika wa mawasiliano kati ya waongoza ndege na marubani.
Pia kuingia mikataba ya usimikwaji wa mitambo ya kutoa taarifa za kidigitali yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 12 itakayotoa taarifa za kidigitali kwa marubani, hali inayolifanya anga la Tanzania kuendelea kuwa salama zaidi hivyo kushawishi wawekezaji, pia ndege nyingi kutumia anga la Tanzania.
Hali inayochagiza kuongezeka mapato ya Serikali pia kuwa na kiwango kidogo cha ajali za ndege.
Hayo yameelezwa leo na Kaimu Mkurugenzi wa huduma za uongozaji ndege, Hamisi Kisesa alipozungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), katika Mkutano wa 43 wa Chama cha Waongoza Ndege nchini (TATCA), jijini Dar es Salaam.
“Viashiria vinaonesha kwamba tuna uwezo mzuri wa kudhibiti anga na kuwezesha huduma za uongozaji ndege zinafanyika kwa viwango vya kimataifa,” amesema Kisesa.
Amesema Serikali hivi karibuni imewezesha kufungwa kwa rada katika Mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mwanza pia Songwe hivyo kufanya anga kuwa salama na kuaminika zaidi kimataifa.
Kwa upande wa elimu kwa waongoza ndege, Kisesa amesema TCAA imekuwa ikiwapa waongoza ndege mafunzo ya mara kwa mara, kwa kutenga bajeti ya asilimia 10 kwaajili ya mafunzo ya ndani, pia kusafiri nje ya nchi ikiwemo Afrika Kusini, Ujerumani, Uganda, Kenya ili kuhudhuria Mikutano ya Kimataifa kwaajili ya kuwaongezea uwezo zaidi.
Kisesa amegusia pia maendeleo ya TATCA na kueleza kuwa “Mwaka 2003 wakati TATCA inaanzishwa kulikuwa na waongoza ndege wasiozidi 50, lakini sasa wanafika waongoza ndege 150 wenye viwango vya kimataifa.”
Naye, Rais wa TATCA, Merkiory Ndaboya amesema ingawa Serikali imekuwa ikiwawezesha katika mafunzo lakini wangependa kupata mafunzo zaidi kwa kuwa mafunzo zaidi huchochea uwajibikaji zaidi.
“Changamoto kubwa tunayokabiliana nayo waongoza ndege ni stress (msongo wa mawazo) ila tunaishukuru mamlaka inatupatia mafunzo ya kumanage stress (kukabiliana na msongo wa mawazo).” Amesema Ndaboya.
Amesema, kiwango cha ndege wanazozihudumia kimekuwa kikiongezeka, kwa mfano kutoka kuhudumia ndege 300 kutoka mwaka 2014 hadi kufikia ndege 400 kwa miaka ya karibuni.