Zaidi ya watu 10,000 wauawa Gaza tangu kuanza vita
ZAIDI ya watu 10,000 wameuawa huko Gaza tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na Palestina mwezi mmoja uliopita, Wizara ya Afya inayodhibitiwa na Hamas katika eneo la Palestina imeeleza.
Israel ilitangaza operesheni dhidi ya Hamas baada kundi hilo la wanamgambo kufanya shambulizi Oktoba 7, na kuua 1,400 nchini Israel na kuwateka nyara zaidi ya 240.
Israel ililipiza kisasi kwa kuanzisha mashambulizi ya anga na ardhini huko Gaza, na kuapa kuliangamiza kundi hilo.
Msemaji wa wizara hiyo, Ashraf Al Qudra amesema Wapalestina 10,022 katika eneo hilo wameuawa na mashambulizi ya Israel, wakiwemo watoto 4,104, wanawake 2,641 na wazee 611.
Idadi hiyo inaonesha takriban robo tatu ya waliokufa ni kutoka kwa watu waliokuwa hatarini. Wizara pia iliripoti majeruhi 25,408. Haijulikani ni wapiganaji wangapi wamejumuishwa kwa jumla.