UNGUJA, Zanzibar: RAIS wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi amesema ujenzi wa bandari mpya ya abiria eneo la Mpiga Duri ni azma ya Serikali kuondoa msongamano katika bandari ya Malindi sehemu ya abiria ambayo ina changamoto ya nafasi.
Dk Mwinyi amesema hayo leo katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ushirikiano kati ya Serikali na kampuni ya ZF DEVCO ya ujenzi wa bandari ya abiria eneo la Mpiga Duri, Ikulu Zanzibar.
Ameeleza kuwa bandari hiyo ya kisasa itakuwa na eneo la boti za abiria, usafiri wa boti za mizigo, taxi za baharini, maduka ya kisasa, ndege zinazotua na kuruka baharini, kituo cha umma cha mabasi, hoteli ya nyota tano, ukumbi wa kimataifa wa mikutano pamoja na eneo la maegesho ya boti.
Vilevile gharama za mradi wa ujenzi huo ni dola za kimarekani milioni 400 , na utakamilika kwa miezi 36 ijayo.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Balozi wa Uholanzi nchini, Wiebe De Boer, Viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya siasa na waandishi wa habari.