Zanzibar na mkakati kurejesha hadhi ya karafuu duniani
ZANZIBAR kuitwa kisiwa cha marashi ya karafuu ni kutokana na uzalishaji wa wingi wa zao hilo. Hivi sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kurejesha hadhi ya zao hilo duniani.
Serikali imesema imejipanga kuongeza uzalishaji wa zao hilo kufikia tani 20,000 kwa mwaka kutoka tani 8,000 kinachozalishwa kwa sasa.
Karafuu katika miaka ya 1960 ilikuwa ndiyo uti wa mgongo wa serikali katika kuingiza fedha za kigeni na uchumi wa Zanzibar, bado linashikilia namba moja ya mazao yanayoingiza kipato kwa serikali na wakulima kwa asilimia 80.
Kisiwa cha Pemba kinaongoza kwa uzalishaji wa karafuu kwani asilimia 90 ya karafuu yote inayozalishwa Zanzibar inatoka Pemba na Unguja huzalisha asilimia 10. Karafuu ya Zanzibar inasafirishwa nje ya nchi kwa wingi.
Uzalishaji wa karafuu umeshuka kwa kiwango kikubwa kutoka tani 20,000 katika miaka ya 1960-78 hadi kufikia kiwango cha sasa tani 8,000 na kushuka katika nchi zinazozalisha na kusafirisha zao hilo.
Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imetangaza mikakati madhubuti ya kurudisha hadhi ya zao hilo katika kiwango cha kimataifa na kufikia tani 20,000 kwa wakulima wa Unguja na Pemba.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi alitangaza mikakati hiyo alipofanya ziara ya kikazi kisiwani Pemba. Alieleza nia ya serikali kuwawezesha wakulima ili kuongeza kasi ya kulima karafuu kwa kuwapatia nyenzo na mikopo yenye masharti nafuu.
Dk Mwinyi aliiagiza Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kushirikiana na Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC) kuhakikisha wanapanga mipango ya pamoja ya kuboresha kilimo hicho kwa wakulima.
Alisema haoni sababu kwa nini Zanzibar ishindwe kuzalisha tani 20,000 za karafuu wakati mazingira ya uzalishaji wa kilimo hicho ni mazuri na wakulima wanaweza kupata bei nzuri ya zao hilo.
“Natoa maagizo kwa Wizara ya Kilimo pamoja na Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC) kuhakikisha kwamba wanakaa pamoja na kupanga mikakati ya kurudisha hadhi ya zao la karafuu katika soko la dunia,” alisema.
Kwa upande mwingine, Dk Mwinyi aliwataka wakuu wa mikoa miwili ya Pemba (Kaskazini Pemba na Kusini Pemba) kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu juhudi zinazochukuliwa na wizara hiyo pamoja na ZSTC kuona uzalishaji wa karafuu unaimarika kwa kiwango kikubwa.
Alisema wakuu wa mikoa wanawajibika kwa kiasi kikubwa katika kufuatilia kuona kazi za uimarishaji wa karafuu kitaifa unaofanyika hatua ambayo itaongezea mapato serikali na wakulima kunufaika.
“Wakuu wa mikoa miwili ya Pemba nataka mfuatilie kwa karibu maagizo yangu ya kuona tunarudisha hadhi ya zao la karafuu kimataifa ambapo tunataka kuona Wizara ya Kilimo na ZSTC wanafanya kazi pamoja katika kuimarisha zao la karafuu kimataifa,” alisema Dk Mwinyi.
Akizungumza na wakulima na viongozi wa Pemba kauli ambayo aliirudia tena katika maadhimisho ya Siku ya Wakulima Nanenane iliyofanyika Kizimbani Dole, Unguja, Dk Mwinyi alisema serikali haina nia ya kulibinafsisha zao la karafuu kuingia katika soko huria kutokana na umuhimu wake.
Alisema karafuu inagusa moja kwa moja maisha ya wananchi na wakulima wake wengi ambao wananufaika kwa kiwango kikubwa pamoja na serikali kwa ujumla wake kwa hivyo hakuna sababu la kulibinafsisha na kuliingiza katika soko huria.
Dk Mwinyi alisema kazi kubwa inayofanywa na serikali kwa sasa ni kuliimarisha ikiwemo kugawa miche ya karafuu kwa wakulima kila inapofika maadhimisho ya Siku ya Wakulima Nanenane.
Alisema wakati umefika wa kuimarisha vitalu vya Wizara ya Kilimo vinavyozalisha miche ya karafuu pamoja na vitalu vinavyomilikiwa na watu binafsi ikiwa ni hatua za kuongeza kasi ya uzalishaji wa zao hilo.
Alisema kwa sasa bei ya karafuu ni nzuri yenye kuvutia katika soko la dunia ambapo serikali inaendelea kununua karafuu kilogramu moja daraja la kwanza kwa Sh 14,000.
“Nataka nitoe ahadi yangu kwamba serikali haitalibinafsisha zao la karafuu kuingia katika soko huria kwa sababu ya umuhimu wake kwa serikali na maisha ya wananchi wetu katika kustawisha kipato chao,” alisema Dk Mwinyi.
Akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Indonesia, Makocha Tembele, visiwani humo, Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kufanya juhudi za kulifufua zao la karafuu kufikia uzalishaji wa tani 20,000 kwa mwaka.
Othman alimtaka balozi huyo kwenda kuongeza ushawishi kwa Indonesia katika suala zima la kuimarisha kilimo cha karafuu na uzalishaji wake pamoja na kazi za utafiti.
Alisema mchango wa Indonesia ni mkubwa katika kilimo cha karafuu kwa kuwa imepiga hatua kubwa katika utafiti na uzalishaji wa karafuu na kwa sasa wanaongoza katika uzalishaji duniani kote.
“Zanzibar tunahitaji kuongeza uzalishaji wa karafuu kufikia tani 20,000, kwa sasa uzalishaji upo katika wastani wa tani 8,000 ambazo ni kidogo, sasa tunahitaji mchango mkubwa katika masuala ya utafiti na ubunifu ambapo wenzetu Indonesia wamepiga hatua kubwa,” alisema Othman.
Historia inaonesha kwamba karafuu iliingizwa Zanzibar kutoka Indonesia katika karne ya 19 na watawala kutoka Oman walioliendeleza zao hilo na kufikia kiwango cha biashara na kusafirishwa nje ya nchi baada ya kuonesha kustawi vizuri.
Wakulima wa karafuu katika Kisiwa cha Pemba kinachoongoza kwa uzalishaji zao hilo wametoa ya moyoni na kuitaka Wizara ya Kilimo pamoja na ZSTC kuongeza ushirikiana wa pamoja ikiwemo upatikanaji wa miche ya karafuu na utafiti wa uzalishaji bora.
Mkulima wa karafuu wa Mtambwe, Pemba jimbo ambalo linazalisha kwa wingi karafuu, Hamadi Issa alisema wanakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa miche mipya ya karafuu waioteshe katika mashamba yao na kupunguza kuwepo kwa karafuu za zamani ambazo wamezirithi kwa wazazi wao.
“Rais Dk Mwinyi ametuambia tuachane na mikarafuu ya urithi…..ni kweli tunakabiliwa na tatizo la uhaba wa miche kwa ajili ya mashamba mapya,” alisema Issa.
Naye Juma Muhamadi, mkulima wa karafuu wa Kijiji cha Chokocho, Wilaya ya Mkoani, Pemba alisema utafiti zaidi unahitajika kwa ajili ya kupata miche ya karafuu yenye uwezo wa kuzalisha karafuu nyingi na bora zaidi.
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Zanzibar, Omar Said Shaaban, akizindua msimu wa mavuno mdogo wa karafuu huko Pemba Kichunjuu Mtambwe, alisema ZSTC katika mwaka 2021-2022 inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia mpango mkakati wa shirika wa miaka mitano 2021-2025 pamoja na mpango wa biashara wa kuongeza kiwango cha uzalishaji wa karafuu.
Alisema katika mwaka 2021-2022 shirika limepanga kununua tani 5,630 za karafuu kavu zenye gharama Sh bilioni 56.3 na hadi kufikia Machi mwaka huu jumla ya tani 8,703 zimenunuliwa kutoka kwa wakulima kwa gharama ya Sh bilioni 113.36.
Shaaban alisema shirika linaendelea kununua makonyo ya karafuu ambayo hutumika kwa ajili ya kutengeneza mafuta ya karafuu ikiwa ni miongoni mwa bidhaa zinazozalishwa na shirika kupitia kiwanda chake cha Makonyo kilichopo Wawi, Pemba.
“Hiyo ndiyo mikakati ya shirika la kuongeza uzalishaji wa karafuu ambapo tayari tumefikia tani 8,703 tukiamini kwamba tunakwenda kuongeza kiwango cha tani kufikia 20,000,” alisema Shaaban.