RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameishukuru Taasisi ya Uturuki ya Iyilik Dernegi kwa kuichagua Zanzibar kuwa kituo kikuu cha kuandaa utekelezaji wa miradi yote kwa nchi za Afrika Mashariki.
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu Zanzibar, ilisema Dk Mwinyi alitoa shukrani hizo alipokutana na kuzungumza na ujumbe wa taasisi hiyo, ulioongozwa na Kaimu Mwenyekiti, Metin Calbay.
Ujumbe huo ulimweleza Dk Mwinyi shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo katika nchi mbalimbali Afrika.
“Serikali imepokea ombi la taasisi hiyo la kupatiwa eneo la ardhi kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho kitakachokuwa na majengo ya shule kuanzia ngazi ya awali hadi sekondari, chuo cha kilimo na ufundi,” alisema.
Dk Mwinyi alifurahishwa na misaada mbalimbali inayotolewa na taasisi hiyo kwa jamii ya Wazanzibari na bara lote la Afrika kwa kutambua kuwa jukumu hilo ni kazi ya serikali.
Awali, Calbay alisema taasisi hiyo ina azma ya kujenga kituo kikuu visiwani humo kwa ajili ya miradi ya kudumu katika nchi za Afrika Mashariki na aliomba serikali kuangalia uwezekano wa kupatiwa eneo hilo ili kufanikisha azma hiyo.
Calbay alisema taasisi hiyo imeshawasaidia wananchi wa Zanzibar kwa kuwapa mbuzi 450 wa maziwa ili wawaendeleze kwenye miradi ya ufugaji na upande wa Tanzania Bara wameshatoa mbuzi 1,550 kwa lengo hilo la kuwainua wananchi kiuchumi kupitia miradi ya ufugaji.