Zelenskyy anusurika ajali ya gari

RAIS wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy yuko salama baada ya gari kugonga msafara wake mjini Kyiv, msemaji wake Serhii Nykyforov amethibitisha kupitia ukurasa wake wa Facebook mapema Alhamisi.

Zelenskyy alikuwa akirejea katika mji mkuu baada ya ziara ya kushtukiza huko Izyum, mji muhimu uliorejeshwa chini ya vikosi vya Ukraine baada ya jeshi ya Urusi kurudi nyuma. Nykyforov amesema Zelenskyy hajapata “majeraha makubwa.”

“Gari liligongana na gari la rais na magari yake ya kusindikiza huko Kyiv,” msemaji wa Zelenskyy alisema. “Rais alichunguzwa na daktari, hakuna madhara makubwa.” Madaktari waliokuwa wakiandamana na Zelenskyy walimpa dereva wa gari hilo msaada wa dharura, kabla ya kumhamishia gari la wagonjwa.

Nykyforov hakusema ni muda gani ajali hiyo ilitokea.

“Mazingira yote ya ajali hiyo yatachunguzwa na vyombo vya sheria,” Nykyforov alihitimisha, bila kuzungumzia nia ya ajali hiyo.

Zelenskyy alitoa muhtasari wa kile kinachoendelea kuhusu mashambulizi dhidi ya vikosi vya Urusi lakini hakutaja tukio la ajali hiyo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button