SERIKALI ya Marekani imeahidi kujenga kiwanda kikubwa nchini Tanzania cha kuchakata madini aina ya nickel yatakayotumika kutengeneza betri za gari ya umeme na kinatarajiwa kukamilika mwaka 2026.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax, wakati akielezea matokeo ya ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris iliyofanyika nchini Machi 29-31 mwaka huu.
Amesema ujenzi wa kiwanda hicho unatarajiwa kutekelezwa na kampuni mbili zinazomilikiwa kwa ubia na serikali ya Marekani kupitia Shirika la Fedha La Kimataifa la Marekani.
Amesema kiwanda hicho kitatoa ajira kwa Watanzania na kitachangia kukuza pato la taifa kwa serikali ya Tanzania
Pia amesema zimesainiwa hati mbili za makubaliano, ikiwa ni mkataba wa msaada wa maendeleo kati ya Tanzania na Marekani kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi pamoja na hati itakayowezesha serikali ya Marekani kutoa ushauri wa kitaalamu, kuwajengea uwezo wasimamizi wa Bandari Tanzania hususani katika upanuzi wa bandari na uendelezaji wake.
Akizungumzia uboreshaji wa afya nchini Tax amesema serikali ya marekani imeahidi kutoa nyongeza ya dola za Marekani milioni 1.
3 kwa ajili ya kuboresha sekta ya afya na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko pamoja na Sh milioni 433 kuwekeza katika mpango wa dharura wa Rais wa kusaidia kupambana na Ukimwi katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

Ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi, biashara na uwekezaji zinazotokana na ushirikiano wa Tanzania na nchi mbalimbali, ikiwemo Marekani na kuunga mkono juhudi za serikali kuleta maendeleo ya Taifa.