Ziara ya kampuni za Kimarekani nchini yazinduliwa

Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara imezindua rasmi ziara ya kampuni za Kimarekani kutembelea Tanzania Bara na Zanzibar kujionea fursa za kibiashara na uwekezaji.

Uzinduzi huo umefanyika leo, Jumanne, jijini Dar es Salaam ambapo takribani kampuni 20 ya Kimarekani zilijisajili kushiriki katika ziara hiyo inayolenga kuangazia biashara za kilimo, nishati, huduma za afya na viwanda vya teknolojia ya habari na mawasiliano.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ziara hiyo, Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Donald Wright aliyapongeza makampuni hayo kwa uamuzi wao wa kuiangalia Tanzania kama mahali pa kuwekeza katika sekta muhimu za uchumi na kupanua biashara zao.

pharmacy

“Tunakaribisha ushiriki zaidi wa Wamarekani katika uchumi wa Tanzania – kwa hakika, hii ni moja ya malengo ya msingi kabisa ya ubalozi wetu. Makampuni ya Kimarekani huja na ubunifu, ujuzi na mtaji lakini pia huja na nia ya kuwafundisha Watanzania jinsi ya kusimamia na kuendesha biashara zao,” alisema Balozi Wright.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, Marekani ni ya tatu miongoni mwa wawekezaji wakubwa zaidi wa kigeni nchini.

“Marekani imekuwa ikitoa msaada wa maendeleo na msaada mwingine katika kujenga uwezo wa kushughulikia masuala ya afya na elimu, kuchochea ukuaji mpana wa uchumi na kuimarisha usalama wa kikanda na wa humu nchini ili kudumisha maendeleo.” alisema waziri Kigahe.

Siku ya kwanza ya ziara hiyo itahusisha kupata maelezo kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Chama cha Wafanyabiashara na Makampuni ya Kimarekani nchini Tanzania na Umoja wa Watendaji Wakuu wa Taasisi nchini Tanzania (CEO Roundtable of Tanzania pia washiriki watakuwa na majadiliano na wawakilishi wa serikali ya Tanzania.

Ziara hiyo imeandaliwa na Vyama vya Wafanyabiashara na kampuni ya Kimarekani (“AmCham”) katika nchi za Kenya, Tanzania and Afrika ya Kusini.

Kwa mujibu wa ubalozi wa Marekani nchini Tanzania siku ya kesho, 28 Septemba, ujumbe wa wafanyabiashara hao utaelekea Zanzibar ambako utapokea maelezo kutoka kwa wawakilishi wa serikali na kufanya majadiliano na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar na kuhudhuria mkutano utakaohutubiwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Othman Masoud Othman.

Habari Zifananazo

Back to top button