Ziara ya Rais Samia nchini India yatabiriwa makubwa

INDIA: WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki January Makamba amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Dk.Subrahmanam Jaishankar ikiwa ni maandalizi ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan atakayoifanya nchini humo kuanzia Oktoba 8 – 11, 2023.
Katika mazungumzo yao yaliyofanyika hivi karibuni jijini New Delhi, viongozi hao pamoja na mambo mengine wamelezea matarajio yao ya kuimarika zaidi kwa ushirikiano kati ya Tanzania na India kupitia ziara hiyo ya kihistoria.
Mawaziri hao walibadilishana taarifa kuhusu ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili na kukubaliana kuongeza jitihada ili kufikia malengo ya pamoja ya kuinua kiwango cha biashara na uwekezaji kati ya nchi hizi mbili na kuhakikisha ushirikiano uliopo unazaa matokeo tarajiwa.
Rais Samia anatarajiwa kuwasili India Oktoba 8, 2023 kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu.
Wakati wa ziara hiyo kutashuhudiwa ubadilishanaji wa mikataba mbalimbali ya ushirikiano katika sekta za uwekezaji, uchukuzi, afya, maji na nyingine nyingi.
Ziara hiyo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na India hususan kwenye maeneo ya kimkakati na manufaa kwa Tanzania ikiwemo afya, maji, elimu uchumi wa buluu, teknolojia, kilimo, na biashara na uwekezaji.

Habari Zifananazo

Back to top button