Ziara ya Samia Qatar kunufaisha uchumi, afya

Ziara ya Samia Qatar kunufaisha uchumi, afya

BALOZI wa Tanzania nchini Qatar, Mahadhi Juma Maalim amezitaka taasisi na sekta zinazohusika kutekeleza haraka makubaliano yaliyofikiwa katika Mkutano wa Ubunifu kuhusu Masuala ya Afya uliofanyika hivi karibuni mjini Doha na kuhudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Aidha, mabalozi wanaowakilisha Tanzania katika mataifa ya Ghuba, wameshauriwa kutumia nguvu na ushawishi wao kuvutia matajiri wanaowekeza fedha nyingi Ulaya kuja kuwekeza Tanzania kutokana na mazingira mazuri yaliyowekwa na serikali kwa wawekezaji.

Balozi Maalim alisema hayo jana katika mkutano ulioandaliwa na Watch Tanzania kwa njia ya mtandao uliojadili masuala yaliyojiri katika ziara za Rais Samia katika mataifa ya Ghuba hususani karibuni nchini Qatar.

Advertisement

Alisema ingawa uhusiano wa Tanzania na Qatar ulianza miaka ya 1980, Rais Samia ndiye kiongozi wa kwanza kuimarisha zaidi uhusiano wa mataifa hayo mawili baada ya kutumia fursa ya Mkutano wa Ubunifu wa Masuala ya Afya kukutana na viongozi wakuu wa nchi hiyo.

“Mkutano ule ulifanya jina la Tanzania kufahamika vyema katika vyombo vya habari nchini Qatar, kufahamika vyema kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Qatar na kufanikiwa kufungua milango ya mafanikio kwa Tanzania,” alisema Balozi Maalim.

Alisema kutokana na juhudi za Rais Samia, idadi ya watu wanaokuja Tanzania kutoka Qatar kwa biashara na utalii imeongezeka hali iliyowezesha kuongeza ndege kutoka mbili hadi nne kwa siku zinazokuja Tanzania.

Alisema Serikali ya Qatar imekubali kuleta wafanyabiashara, wawekezaji na watalii baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia zinazotarajiwa kuanza Novemba 21, mwaka huu nchini humo.

Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, Saidi Mussa alisema matajiri wengi wa mataifa ya Ghuba wamewekeza katika mataifa ya Ulaya kutokana na propaganda iliyofanywa na mataifa hayo kuwa Afrika sio mahali salama pa kuwekeza.

Aliwataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa ya Ghuba, kutumia akili zao na uwezo wao kuhakikisha wanazima uzushi na propaganda hizo.

Amewataka kuhakikisha sera na mazingira mazuri ya uwekezaji ya Tanzania yanafahamika ili kuwashawishi kuacha kupeleka fedha zao Ulaya na badala yake wazilete Tanzania.

Naibu Waziri wa Afya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hassan Khamis Hafidh alisema mafanikio ya mkutano huo ni makubwa na kwamba Tanzania imejifunza kutoka Qatar kwa kuwa ni taifa lililoendelea vizuri katika ubunifu na sekta ya afya.

Alisema mafanikio ya mkutano huo kwa Tanzania na Afrika ni pamoja na kuitaka Afrika kuwa na Shirika la Dawa la Afrika (AMA) ili kujitosheleza na si kuwa mtegemezi wa mashirika ya nje huku Qatar ikikubali kushirikiana na Afrika kuwezesha kupatikana kwa shirika hilo.

Aidha, alisema Qatar imekubali kupokea wanafunzi wa masomo ya afya na pia imekubali kujenga Jengo la Mama na Mtoto na kuleta wataalamu kutoa mafunzo kwa wataalamu wa Tanzania kuimarisha ujuzi wao.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), John Mali alisema wamelitenga eneo la Mashariki ya Kati kama eneo lao la kimkakati ili kutumia fursa za uwekezaji, biashara na utalii kuinufaisha Tanzania.

Alisema kituo hicho kimejipanga kutumia fursa zilizopatikana katika mkutano huo pamoja na fursa zilizopatikana katika Mkutano wa Dubai kwenye Kongamano la Biashara la Dubai Expo.

/* */