Jeshi la Zimamoto na uokoaji mkoani Arusha limewaonya wananchi wanaotoa taarifa za uongo kwa jeshi hilo, likisema linahitaji ushirikiano kutoka kwa wananchi, lli liweze kutimiza malengo yake
Limesema pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na jeshi hilo mkoani Arusha kwa kutoa elimu kwa wananchi, bado kuna changamoto kubwa ya watu wasiokuwa na nia njema wanapiga simu na kutoa taarifa za uongo ofisi za jeshi hilo za majanga
Akizungumza na HabariLEO, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Arusha, Osward Mwanjejele amesema kwamba taariza za uongo wanazozipokea kutoka kwa watu mbalimbali jijini Arusha zinazilifedhehesha jesho hilo
“Kwa kweli taarifa za majanga kutoka kwa watu wasiowaaminifu, zinatufedhehesha sana maana tunatumia rasilimali zetu na nguvu nyingi kwenda kwenye tukio. Unapofika kwenye tukio hukuti chochote,” amesema
Amesema katika kipindi cha miezi ya karibuni jeshi hilo lilipokea simu 8 kutoka kwa watu mbalimbali wakilifahamisha jeshi hilo kuwa kuna matukio ya majanga.
“Watu watupe ushirikiano, wasipambane na matukio na watoe taarifa za kweli,” alisema
Amesema kwamba karibu mwaka mzima jeshi hilo limekuwa likitoa elimu kwa umma kuhusu masuala yanayohusu majanga ya moto na uokoaji katika Mkoa wa Arusha.
“Tumekuwa tukitumia vyombo vya habari hasa magazeti, redio na televisheni katika kutoa elimu kwa umma. Pia tunatumia na majukwaa mbalimbali kama vikao vya madiwani, kwenye maonesho na pia wakati mwingine huwa tunaalikwa kwenye mikutano ya serikali za mitaa,” amesema.
Pia ametoa ushauri kwa wananchi kuchukua tahadhari mapema na kuepukana na matumizi holela ya mitungi ya gesi nyumbani, pia katika uchimbaji wa visima ambavyo wakati wa mvua vinajaa maji na kusababisha vifo.