Zimbabwe kusitisha mikopo fedha za kigeni

RAIS wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa ameamuru Benki Kuu nchini humo kusitisha kukopa fedha za kigeni kutoka vyanzo vya nje, hatua ambayo imechukuliwa wakati serikali inapambana kudhibiti kuporomoka kwa thamani ya fedha ya nchi hiyo kuelekea uchaguzi mkuu ambao utafanyika mwezi Agosti mwaka huu.
Mnangagwa ambaye anatupa karata yake kuwania tena urais Agosti 23 anakabiliwa na mchuano mkali huku ongezeko la mfumuko wa bei na kushuka thamani ya pesa ya zimbabwe kwa zaidi ya asilimia 80% tangu kuanza kwa mwaka huu.
“Benki ( Kuu ) itakopa tu fedha za kigeni kwa niaba ya serikali kupitia ruhusa ya Waziri wa (Fedha) na sio kuamua tu kwa niaba yake,” Mnangagwa alisema katika taarifa yake.
Wachambuzi wa masuala ya fedha nchini humo wamedai kuwa mojawapo ya sababu zinazopelekea changamoto hiyo ya sarafu kushuka thamani ni ukopaji wa fedha za kigeni ambao haupo chini ya uangalizi wa bunge unaofanywa na Benki Kuu hatua ambayo imepelekea Serikali ya Zimbabwe kutangaza mikakati ya kuleta uimara wa dola ya zimbabwe na kudhibiti mfumuko wa bei ikiwa ni pamoja na kuhamisha baadhi ya majukumu ya benki kuu kwenda Wizara ya Fedha.