‘Zimebaki rada mbili tu kufikia lengo la serikali’

DODOMA: MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imekamilisha ufungaji wa rada za hali ya hewa katika Mkoa wa Kigoma na Mbeya, hivyo kufikisha jumla ya rada tano za hali ya hewa nchini.

Huku utengenezaji wa rada nyingine mbili unaendelea kiwandani nchini Marekani na inatarajiwa kukamilika mwezi Novemba, 2024.

Akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi bungeni jijini Dodoma ya mwaka wa fedha 2024/2025 Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema Rada hizo zitafungwa katika mikoa ya Kilimanjaro na Dodoma na hivyo kukamilisha lengo la muda mrefu la kuwa na rada saba za hali ya hewa nchini.

WAZIRI wa Uchukuzi, Prof Makame Mbarawa

Prof. Mbarawa amesema katika kuhakikisha mitambo yote inakuwa ya kisasa tayari serikali imeingia mkataba wa kuboresha rada za hali ya hewa zilizofungwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza ambayo ilikuwa katika mfumo wa analogia.

“Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na kujenga uwezo kwa watumishi, Serikali kupitia TMA imeendelea na ujenzi wa jengo la ofisi ya Kanda ya Mashariki na Kituo cha Tahadhari ya Matukio ya,” amesema Prof. Mbarawa.

Soma pia: https://habarileo.co.tz/tma-yangara-miaka-miwili-ya-rais-samia/

Katika hotuba yake hiyo, Mbarawa ameendelea kusema kuwa TMA inaendelea kufanya tafiti mbalimbali za masuala ya hali ya hewa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi ikilenga kuboresha utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini, ambapo jumla ya tafiti nne zilichapishwa katika majarida ya kimataifa ya kisayansi. Idadi hii inafanya tafiti zilizochapishwa na majarida ya kimataifa kuwa nane ndani ya kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2022/23 hadi 2023/24.

Tafiti hizo ni kuhusu tathmini ya matukio ya hali mbaya ya hewa katika Bahari ya Hindi; tathmini ya ongezeko la joto kwa kipindi kati ya mwaka 1982 hadi 2022; tathmini ya hali ya mvua katika vituo vya hali ya hewa nchini; na tathmini ya mabadiliko ya mvua na athari zake katika kilimo kwa nchi za Afrika Mashariki.

Kutokana na umahiri katika utoaji wa huduma za hali ya hewa, mwaka 2019 Shirika la Hali ya Hewa Duniani liliichagua Tanzania kupitia TMA kuendesha kituo cha kanda cha kutoa mwongozo wa utabiri wa hali mbaya ya hewa ‘Regional Specialized Meteorological Centre’ kwa nchi zilizopo katika ukanda wa Ziwa Victoria, ambacho kipo Dar es Salaam na kinahudumia nchi tano (5) ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, na Burundi.

Habari Zifananazo

Back to top button