‘Zingatieni kiapo cha uaminifu kutunza siri’

RAIS Samia Suluhu Hassan, amewataka watunza kumbukumbu na nyaraka (TRAMPA) na makatibu mahsusi (TAPSEA) kuzingatia kiapo cha uaminifu katika kutunza siri kwa kuwa kina maana kubwa katika utendaji wa kazi zao.

Akizungumza leo Mei 27, 2023 visiwani Zanzibar, akifunga mafunzo ya uadilifu kwa utunzaji siri kwa watunza kumbukumbu na nyaraka na makatibu mahsusi, Rais Samia amewataka kuzingatia nidhamu na uadilifu kwa kuwa mambo hayo mawili yanazaa ufanisi.

“Ufanisi maana yake ni kuikamilisha kazi vile inavyotakiwa, kwa kiwango kinachotakiwa na wakati unaotakiwa. Ukiwa na nidhamu na uadilifu utazalisha kazi kwa wakati kwa kiwango kinachotakiwa na muda unaotakiwa,”amesema na kuongeza kuwa kiapo cha uaminifu cha kutunza siri walichokula mbele ya Wakili Mkuu wa Serikali na yeye kushuhudia wakizingatie kwa kuwa kina maana katika utendaji kazi wao wa kila siku.

“Sasa kati yenu mtu akienda kinyume na kiapo chake alichokula akishuhudiwa na Rais wa nchi, tutajuana huko mbele kwa mbele, kwa hiyo naomba muishi kiapo chenu,”amesema.

Pia Rais Samia amesema ni muhimu kwa waajiri na wakuu wa taasisi katika sekta ya umma na sekta binafsi kuwaruhusu watunza kumbukumbu na nyaraka na makatibu mahsusi kushiriki mafunzo ya uadilifu na utunzaji siri, ili kuwajengea uwezo na ufanisi katika kazi zao.

Habari Zifananazo

Back to top button