DAR ES SALAAM; NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Dotto Biteko amesema mafunzo waliyohitimu maofisa wa polisi yakawe chachu ya maendeleo kwa watu na kulipa heshima Jeshi la Polisi na nchi.
Ametoa kauli hiyo baada ya kupokea gwaride maalum la maofisa wapya waliohitimu mafunzo ya Uofisa Kozi No. 1/2022/2023 yenye lengo la kuimarisha kiwango cha utendaji kazi katika Jeshi la Polisi nchini, katika mahafali ya kufunga kozi hiyo leo Novemba 16, 2023 Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini, Dar es Salaam.
Pia amewataka wahitimu hao wakatatue matatizo ya Watanzania na kuwapa huduma, wasione fahari kwa vyeo walivyonavyo na wakakatae rushwa, wasimamie haki kwa wananchi .
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesema jamii imekuwa ikikumbana na changamoto ya maadili kna kusababisha kuharibu sekta mbalimbali, hivyo mafunzo hayo yatawajenga askari hao kufanya kazi kwa uadilifu.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Camillus Wambura amesema jeshi la polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama wana haki ya kudumisha amani nchini.
Katika mafunzo hayo wamehitimu wanafunzi maafisa wapya 952 katika chuo hicho, ambapo yalianza Februari 14, 2023.