Zitto ashauri wakurugenzi wateuliwe na bodi

ARUSHA: Wakati Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa zamani Profesa Mussa Assad akipendekeza Wajumbe wa bodi za mashirika ya umma kufanyiwa usaili, Mwanasiana na Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo amependekeza Watendaji wa mashirika hayo wateuliwe na bodi.

Zitto Kabwe amesema pia wakati akiwasilisha mada katika Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma kuwa Tanzania inapaswa kuwa na sera ya mashirika ya umma ambayo inaaksi mahitaji ya sasa na mabadiliko ya uchumi, siasa, sayansi na teknolojia.

“Kuna haja sasa ya kuhakikisha Wenyeviti wa Bodi wanateuliwa na Mamlaka za Uteuzi, kwa maana ya Rais. Hata hivyo, Mkurugenzi ateuliwe na Bodi ili aripoti kwa Bodi,” amesema Zitto akifafanua kuwa ilivyo sasa Wakurugenzi wanateuliwa na chombo kile kile kinachoteua Wenyeviti.

“Utaratibu ni kwamba ikiwa bodi haitaridhika na utendaji wa Mkurugenzi iwe na nguvu ya kumbadili mkurugenzi … hali hii itaongeza ufanisi,” amesema Zitto ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC).

Akifafanua kuhusu umuhimu wa kuwa na Sera ya Mashirika ya Umma, Mwanasiasa huyo amesema Tanzania haina Sera ya Mashirika ya Umma na kwamba imekuwa ikisimamia mashirika hayo kupitia Sheria ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1992. Sheria hiyo inafanyiwa marekebisho kila uchwao, amesema akishauri kutungwa kwa sheria na sera mpya kuendana na mabadiliko ya uchumi nchini.

Habari Zifananazo

Back to top button