Zitto: Siasa isikwamishe maendeleo

KIGOMA; KIONGOZI wa chama cha ACT Wazalendo ,Zitto Kabwe amewataka viongozi wa vyama vya siasa na wanachama wao mkoani Kigoma kuungana kupigania maslahi na mustakabali wa mkoa huo na wananchi wake badala ya majukwaa ya kisiasa kuwa kikwazo cha maendeleo ya mkoa.
Zitto ametoa kauli hiyo wakati akihitimisha ziara yake ya siku 14 kukutana na viongozi wa chama hicho kwenye Kata zote za Mkoa wa Kigoma na kufanya mikutano ya hadhara katika majimbo manane ya mkoa huo.
Kiongozi huyo amesema kuwa ipo miradi ambayo ilikuwa itekelezwe na benki ya Dunia ukiwemo mradi wa umwagiliaji bonde la Mto Luiche ambayo ilikwama kutekelezwa wakati ACT ikiongoza manispaa na sasa baada ya jitihada kubwa mradi huo umepata idhini kutekelezwa hivyo siyo vizuri siasa kuhamishiwa kwenye kukwamisha maendeleo.
Alisema kuwa Mkoa wa Kigoma bado uko nyuma kimaendeleo hivyo kuwekeana fitina na kufanya miradi kushindwa kutekelezwa siyo tu inawaumiza watu wa chama kimoja bali athari hiyo ni kwa watu wote mkoani humo na kwa taifa kwa jumla.