Zogo laibuka uchaguzi madereva bajaji Katavi

MADEREVA bajaji Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi, wamegomea uchaguzi wa kumpata Mwenyekiti wa Kijiwe cha Bajaji Soko Kuu, kwa madai kuwa majina yaliyopendekezwa si ya madereva kutoka kijiwe hicho.

Wakizungumza na HabariLeo, madereva hao wamedai kuwa, majina yaliyopendekezwa ni hujuma kutoka kwa uongozi wao wa juu, ambao unataka kuingiza watu wake kutokana na uongozi huo kutokubaliana na mapendekezo ya katiba.

“Wameona tumewabana kwenye katiba mpya, wakaona sasa viongozi wa soko kubwa ndio wenye viherehere, kwa hiyo wameona wavunje ule uongoz,i ili sasa wabaki huru, wachague wanaowataka wao, ” amesema Said Juma mmoja wa madereva wa kituo cha Soko kuu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kituo cha waendesha Bajaji Soko kuu, Layson Kang’ombe, amesema hana shida na uongozi wa juu, yeye binafsi pamoja na madereva wa kijiwe hicho, bali utaratibu wa uchaguzi umevunjwa na hawakuwa na taarifa za kufanyika uchaguzi katika kijiwe hicho.

“Vijana wanaomba waite Mkutano Mkuu, ili kama kuna upungufu wa kiongozi yoyote, hata mimi niko tayari, ila wakubali twende kwenye mkutano mkuu, uongozi wa ngazi yote uvunjwe, kuanzia wao vijana wachague upya,”- amesema Kang’ombe.

Kwa madai ya madereva hao, katiba ndiyo chanzo cha mvutano huo, hivyo wanataka uitishwe Mkutano Mkuu utakaopendekeza na kupitisha katiba mpya itakayowaongoza kupata viongozi.

 

Habari Zifananazo

Back to top button