Zoran awashusha presha Simba

KOCHA Mkuu wa Klabu ya Simba, Zoran Maki amewataka mashabiki kutokuwa na wasiwasi na matokeo mabaya ya mechi za kirafiki kwani timu yake inajengeka.

Simba jana ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya As Art Solar ya Djibouti na kufungwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Hicho ni kipigo cha pili mfululizo katika mechi za kirafiki ambapo katikati ya wiki hii ilifungwa bao 1-0 na Al Hilal ya Sudan ilipokwenda nchini humo kwa mwaliko maalumu ambapo ilicheza mechi mbili, moja ikishinda mabao 4-2 dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana.

Akizungumza na gazeti hili baada ya mechi ya jana, Zoran alisema mashabiki wa Simba hawana haja ya kuwa na presha kwani mechi hizo zinafanya kikosi chake kiimarike na kumwonesha kwenye mapungufu arekebishe.

“Nikizizungumzia mechi mbili tulizocheza Sudan zilikuwa ni kipimo sahihi kutokana na mashindano yanayotukabili, ukweli timu imeimarika tofauti na ilivyokuwa mwanzo ingawa bado kuna mapungufu katika baadhi ya nafasi ingawa hilo siyo tatizo sana sababu kadri siku zinavyokwenda ndio tunazidi kuimarika.”

“Kuhusu uwezo wa wachezaji katika mechi tatu za kirafiki nimejitahidi kumpa nafasi kila mchezaji, wapo ambao wamebadili mawazo yangu kwa kiasi fulani nitajitahidi kwa kushirikiana na wenzangu kuwaweka katika ubora ninaoutaka ili tuweze kufikia malengo ya timu,” alisema Zoran.

Kocha huyo raia wa Serbia alisema katika mechi hizo tatu walipoteza mechi mbili dhidi ya Al Hilal na AS Art Solar ya Djibout, kwake matokeo hayakuwa kipaumbele alichokuwa anaangalia ni mbinu na mifumo ambayo amewaelekeza wachezaji wake kama wanayafanyia kazi.

Aidha, Zoran alisema katika mchezo wa jana hakuridhishwa na safu yake ya ushambuliaji hasa mshambuliaji, Dejan  Georgijevic ambaye alipoteza nafasi nyingi za wazi katika mchezo huo.

Alisema yeye akiwa kama kocha mkuu wa timu hiyo atajitahidi kumrekebisha  mshambuliaji huyo ili aongeze umakini na kupunguza papara ili kuzitumia vyema nafasi wanazotengeneza.

Simba ndio inaongoza Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi sita sawa na Yanga na Singida Big Stars zilizo nafasi ya pili na ya tatu. Ligi Kuu iliyosimama kwa takribani wiki mbili inatarajiwa kuendelea wiki ijayo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button