KOCHA Mkuu wa Simba, Zoran Maki ame wapongeza wachezaji wake kwa kupambana na kuvuna pointi tatu dhidi ya Kagera Sugar katika mechi ya Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Huo ni mchezo wa pili Simba kushinda tangu ligi ianze baada ya kushinda mabao 3-0 dhidi ya Geita Gold kwenye Uwanja huohuo.
Akizungumza baada ya mchezo huo wa juzi kocha huyo alisema anavutiwa na namna wachezaji wake walivyojituma kupata ushindi uliowaweka kileleni ingawa bado hajaridhika na kiwango chao. “Ulikuwa ni mchezo mgumu kwetu Kagera walicheza vizuri na kuziba nafasi zote lakini nawapongeza wachezaji wangu kwa kujituma na kutumia uzoefu wao kupata ushindi ambao umeturudisha kileleni mwa msimamo wa ligi,” alisema Zoran.
Alisema, hajafurahishwa na kiwango lakini hilo hawezi kulaumu sana kwakua bado yupo katika mwendelezo ya kujenga timu. Alisema kitu cha msingi kwa sasa ni pointi tatu na wachezaji kuwajibika ndani ya kiwanja na hilo ndio linalofanyika kwa sasa na amewataka mashabiki wa timu hiyo kuwa wavumilivu kipindi hiki.
Alisema falsafa zake ni kuiona Simba siyo inapata ushindi bali kutoa burudani kwa mashabiki ambao wamelipa kiingilio uwanjani kuwashangilia. Aidha kocha huyo alimwagia sifa mshambuliaji Djean Georgijevic kwa kuanza kuzoea ushindani uliopo kwenye ligi ya Bara.
Alisema bao alilofunga anaamini litamuongezea ari ya kupambana ili kuingia kwenye kikosi cha kwanza na hana shaka naye kutokana na anavyo mfahamu.