DODOMA: Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mussa Hassan ‘Zungu’ amemtaka Mbunge Anatropia Theonest kuacha kutumia programu ya Google kutafuta taarifa.
“Umesikia Anatropia….umesikia Anatropiaaaa!. Acha ku-google. ku google hovyo hovyo ikiwa bado hujapata taarifa sahihi juu ya jambo fulani,” amesema Zungu
Zungu ametoa kauli hiyo leo Agosti 6, 2024 bungeni mjini Dodoma baada ya Mbunge huyo wa Viti Maalum (asiye na chama), Anatropia Theonest kuitaka serikali kutenga bajeti maalum ya vifaa vya wajawazito wakati wa kujifungua.
Anatropia pia alidai kuwa kuwa Tanzania ni kati ya nchi tano chini ya jangwa la Sahara zinazoongoza kwa vifo vya wajawazito akieleza vinasababishwa na magonjwa ya kuambukiza wakati wa kujifungua na kutaka kutengwa fungu la vifaa vya kina mama kujifungulia.
“Kwanini vifaa vya kujifungulia visitolewe bila malipo kwa wajawazito ili kupunguza kiwango cha magonjwa ya kuambukiza wakati wa kujifungua?” alihoji.
Akijibu hoja ya Anatropia, Naibu Waziri wa Tamisemi, Dk Festo Dugange amesema Tanzania suala la kijifungua na kifo si kwamba yapo karibu kama anavyosema mbunge huyo wa Viti Maalum.
“Ikumbukwe mwaka 2016 kushuka chini kulikuwa na vifo vya wajawazito 556 kati ya vizazi hai 100,000 lakini hivi sasa baada ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kujenga hospitali, vituo vya Afya na Zahanati, kupeleka vifaa muhimu na dawa vifo vya wajawazito vimepungua kutoka 556 hadi 104 kati ya vizazi hai 100,000,”amesema Dugange na kuongeza
“Unaweza kuona kasi ya vifo vya wajawazito imepungua, kwa uwekezaji mkubwa uliofaywa, Wizara ya Afya na Tamisemi tuna uhakika Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi ambazo zitakuwa na vifo vichache duniani,”amesisitiza.
Aidha, amesema vifaa vya kujifungulia utolewa bure kwa wajawazito wote kwenye Zahanati na Vituo vya Afya, na kwamba wajawazito wanashauri kuwa na vifaa vyao binafsi kama dharura.
Akichangia hoja hiyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Mipango na Uwekezaji, Prof Kitila Mkumbo amesema takwimu zilizopo lengo la miaka mitano ifikapo mwaka 2025 Tanzania iwe imepunguza vifo na kufikia 265.
“Lakini tunazungumzia miaka miwili kabla tunazungumzia vifo 104, kwa hiyo tumekamilisha lengo kabla ya muda, Ukanda wa Afrika Mashariki nchi yetu ndio yenye vifo vichache.”Amesema Kitila
Baada ya hoja hizo, ndio Naibu Spika Zungu akamkanya Anatropia kutotafuta taarifa Google.