Zungu ataka udhibiti mapato bandari Dar

Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azan Zungu

NAIBU Spika wa Bunge, Mussa Azan Zungu ametaka mifumo ya makusanyo katika Bandari ya Dar es Salaam iunganishwe ili kudhibiti upotevu wa mapato.

Zungu alitoa kauli hiyo bungeni Dodoma Jumatano baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, ambako alitoa ushauri wa masuala manne.

Alishauri serikali ihakikishe inaunganisha mfumo wa kukusanya mapato katika Bandari ya Dar es Salaam ili kudhibiti upotevu wa mapato.

Advertisement

“Lipo jambo ambalo halijakaa vizuri huko serikalini, hasa mfumo wa ukusanyaji mapato. Limepigiwa kelele na Rais, Spika na sisi wote tunalipigia kelele, lakini bado inaelekea mnavutana, na kuendelea kuvutana ni kukosa mapato,” alisema Zungu.

Alisema ukusanyaji wa mapato katika Bandari ya Dar es Salaam ni Sh bilioni 95 kwa mwezi wakati bandari moja ya nchi jirani wanakusanya takribani Sh bilioni 300 kwa mwezi.

Alimwomba Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye afanye mabadiliko kuhakikisha fedha zinazopatikana kwa kutumia huduma za intaneti na za watoa huduma ambazo zote kwa sasa zinalipwa nje ya nchi, zibaki nchini.

Alisema wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango wanaweza kuweka mkakati maalumu ili mapato yatokanayo na intaneti na mapato ya watoa huduma ya intaneti nchini yasilipwe nje ya nchi.

Naibu Spika alisema kwa kufanya mabadiliko hayo, nchi itapata fedha nyingi kwenye mawasiliano kupitia huduma ya intaneti ambayo ina fedha nyingi zaidi kupitia data kuliko fedha zinazopatikana kupitia sauti.

Alishauri huduma ya intaneti inaweza kugatuliwa katika maeneo mengi nchini ili vijana watoe huduma hiyo.

Alisema anajua hilo si jambo dogo, litapigwa vita sababu hiyo ni biashara. Alisema anazungumza hilo kwa maslahi ya nchi, ili Rais apate mapato na vijana nchini wapate ajira kutokana na kutoa huduma hiyo.

Katika hatua nyingine, Zungu ameonya wanaoichafua serikali kwamba inachukua makato makubwa kutoka kwenye miamala, wachunguze kwanza miamala hiyo ili kujua inachukua kiasi gani ukilinganisha na kiasi kinachochukuliwa na mabenki na mitandao ya simu.

Alisema serikali ilipunguza gharama na miamala, lakini wananchi wanalalamikia serikali kwamba inapata makato makubwa kutoka kwenye miamala, lakini hawatazami mapato yanayokatwa na benki na kampuni za simu.

Hivyo, alishauri awepo mdhibiti wa kuangalia kiasi cha miamala na cha utoaji wa huduma ili kujua makato hayo badala ya baadhi ya watu kufanya hujuma na kuilaumu na kuichafua serikali inayochukua mapato madogo zaidi.

“Ni vema kukawa na uratibu wa utoaji wa huduma hizo, kwani serikali imekuwa ikichukua fedha kidogo wakati ndiyo inayotoa huduma kwa umma za ujenzi wa vituo na shule, huku mabenki yakichukua fedha nyingi,” alisema Zungu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ilala.

“Lazima ku-regulate (kudhibiti) ili mapato ya mabenki yawe regulated (yadhibitiwe),” alisema.

Aliwataka wabunge kuangalia karatasi ya makato wanapofanya miamala ya kutuma fedha kupitia benki au mitandao ya simu, kufahamu kiasi gani benki na mitandao ya simu inachukua na serikali inachukua kubaini ukweli.