Mbinga yaanza ukarabati barabara

RUVUMA: MKURUGENZI Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Joseph Kashushura, ametangaza mpango wa kurekebisha na kuimarisha miundombinu ya barabara, akilenga zaidi barabara zilizopata athari kubwa kutokana na mvua zilizonyesha msimu uliopita.

Hatua hiyo inakuja baada ya greda la halmashauri kufanyiwa matengenezo na kukamilika, tayari kuanza kazi katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri hiyo ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa mazao kutoka mashambani kwenda sokoni.

Kashushura amesema hayo leo kwenye kikao kazi na watendaji wa kata na maofisa maendeleo ya jamii katika ukumbi wa halmashauri huku alisisitiza umuhimu wa viongozi hao kutoa ushirikiano wa karibu na usimamizi wa hali ya juu wakati wa matengenezo ya barabara hizo katika maeneo yao.

“Mwezi wa nane tunatarajia kuanza kukarabati barabara korofi ambazo zimekuwa changamoto kwa wananchi,”alisema Kashushura.

Miongoni mwa barabara tulizozipa kipaumbele awamu ya kwanza ni Mkurumusi kwenda Lukarasi, barabara ya Kiwombi Kata ya Amani Makoro, Lukiti, Linda kisha tutaelekea maeneo mengine kadiri ratiba zitakavyoelekeza.”Alieleza Kashushura.

Katika hatua nyingine, mkurugenzi aliwataka watendaji kuhakikisha kuwa watendaji wa vijiji wanasoma mara kwa mara taarifa za mapato na matumizi mbele ya wananchi ili  kuongeza uwazi na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi juu ya masuala mbalimbali yanayoendelea katika maeneo yao.

Aidha, amewataka watendaji hao wametakiwa kusimamia kikamilifu utendaji wa kazi katika ofisi zao, ikiwa ni pamoja na kujaza mipango kazi kwenye mfumo wa upimaji utendaji kazi wa watumishi wa umma (PEPMIS), kwani mfumo huo unatoa manufaa makubwa kwa maendeleo ya mtumishi binafsi na taaluma yake.

Naye, Mkuu wa Divisheni ya Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu, Hamisi Mkelle aliwataka watendaji hao na watumishi wengine wa halmashauri kufanya kazi kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo ya utumishi wa umma.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button