Miaka 15 ya mgogoro wa ardhi, serikali yaingilia kati

ARUSHA: Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya, amewataka wananchi wa Monduli na Simanjiro kufafanua kwa kina namna na wakati mwekezaji wa Maasai Stepple Conservancy Ltd alivyopatiwa Shamba Na. 24 lenye ukubwa wa hekta 3,425, ili kupata msingi wa kutatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa takribani miaka 15.

Mmuya alitoa kauli hiyo jana katika Ofisi ya Kijiji cha Oldonyo, Kata ya Lemoot, Wilaya ya Monduli, alipokutana na wananchi wa kijiji hicho pamoja na wakazi wa Kijiji cha Lobusoit A, Wilaya ya Simanjiro, ambao kwa pamoja wamekuwa wakilalamikia umiliki na matumizi ya eneo hilo.

Amesema kujenga uelewa wa pamoja kuhusu chanzo cha mgogoro huo ni hatua muhimu katika kutafuta suluhisho, ikiwemo kushughulikia madai ya wananchi ya kurejeshewa maeneo wanayodai kupoteza.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa katika kikao hicho, wananchi wa Monduli wanadai eneo la hekta 870.3, huku wale wa Simanjiro wakidai hekta 1,778.3, kati ya jumla ya hekta 3,425 zinazohusishwa na umiliki wa mwekezaji huyo


“Tunataka kujenga uelewa wa pamoja wa chanzo cha mgogoro huu ili kupitia uelewa huo tujenge hoja ya kupata suluhisho,”

Mgogoro huo, unaodaiwa kuanza mwaka 2011 baada ya mwekezaji kumiliki shamba hilo, umedumu kwa takribani miaka 15 na umeendelea kuwa chanzo cha malalamiko kutoka kwa wananchi wanaotegemea eneo hilo kwa shughuli mbalimbali, hususan ufugaji.

Mbunge wa Monduli, Isack Joseph amema wananchi wa Monduli na Simanjiro wanahitaji ardhi yao na kwamba suluhisho la mgogoro huo linapaswa kurejesha matumaini na amani kwa pande zote.

“Monduli tunahitaji ardhi, na Simanjiro wanahitaji ardhi; sote tunahitaji ardhi irudi mikononi mwetu,”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Oldonyo, Saitoti Mwatuni, amemuomba Naibu Waziri kuupa mgogoro huo kipaumbele ili suluhisho lipatikane kwa haraka kwa ni kijiji hicho kinategemea kwa kiasi kikubwa eneo hilo kwa ajili ya malisho ya mifugo, hivyo kuendelea kwa mgogoro huo kunaathiri maisha ya wananchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button