Kampuni yashinda tuzo Tehama

DAR ES SALAAM: Kampuni ya Mainstream Group Limited imeshinda tuzo mbili katika Tuzo za Tehama Awards 2026, ikiwemo nafasi ya pili katika kipengele cha Ubunifu wa Teknolojia katika Mifumo ya Malipo, huku Mkurugenzi wake, Deogratius Lazari Mosha, akitambuliwa miongoni mwa viongozi bora wa kampuni zinazofanya vizuri katika sekta ya TEHAMA nchini.
Tuzo hizo zimetolewa usiku wa Agosti 9, 2026 kDar es Salaam, katika hafla iliyowakutanisha wadau wa teknolojia na uchumi wa kidijitali. Mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Angela Kairuki.
Katika kipengele cha Ubunifu wa Teknolojia katika Mifumo ya Malipo, Mainstream Group imepata nafasi ya pili baada ya kushindanishwa na taasisi mbalimbali, ikiwemo NMB Bank. Tuzo hiyo inaangazia jitihada za kutumia teknolojia kuboresha na kurahisisha huduma za kifedha.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Deogratius Lazari Mosha, ametambuliwa kutokana na mchango wake katika sekta ya TEHAMA.
Mosha pia aliwahi kutunukiwa tuzo ya Kiongozi Bora katika Ubunifu Barani Afrika mwaka 2024 kupitia tuzo za Forty Under 40 Africa zilizoandaliwa na Xodus Communications Limited.

Hii ni mara ya pili kwa Mainstream Group kutambuliwa katika Tuzo za Tehama nchini Tanzania. Mwaka 2024, kampuni hiyo ilishinda tuzo katika kipengele cha Ubunifu katika Matumizi ya TEHAMA kwenye Sekta ya Fedha.
Ushindi huo umekuja miezi kadhaa baada ya kampuni hiyo kushinda zabuni ya kutengeneza mfumo wa usajili wa wanachama wa Simba Sports Club, unaolenga kurahisisha mchakato wa usajili wa wanachama na utoaji wa kadi zao.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mainstream Group, Pascal William, amesema kutambuliwa huko kunatoa msukumo wa kuendelea kutengeneza mifumo inayolenga kutatua changamoto katika sekta mbalimbali, ikiwemo huduma za kifedha na elimu ya juu.
William amesema kampuni hiyo imeshiriki katika utengenezaji wa mifumo ya kurahisisha huduma za benki pamoja na mifumo ya elimu katika vyuo vikuu, ikiwemo Smarti Uni.
Amesema shughuli hizo zimekuwa na mchango pia katika ajira kwa vijana, ambapo kampuni hiyo inatoa ajira rasmi na zisizo rasmi kwa zaidi ya vijana 100 nchini, sambamba na kuchangia mapato ya Serikali kupitia kodi.



