Rais Samia afurahishwa huduma NSSF

ZANZIBAR; Rais wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, ametembelea banda la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika Tamasha la Kizimkazi, ambapo alipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba.

Pamoja na kutembelea banda la Mfuko, Rais Samia pia alitembelea mabanda mengine ya taasisi na kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa.

Akiwa kwenye Banda la NSSF, Rais amefurahishwa na kazi nzuri inayofanywa na NSSF hususan katika kuboresha huduma kwa wanachama.

Katika hatua nyingine,  NSSF imeendelea kutekeleza wajibu wake kwa jamii katika maeneo ya elimu, afya, michezo, jamii, mahitaji maalum na wadau wa maendeleo.

Katika tamasha la Kizimkazi, Mfuko umewajibika kwa jamii kupitia utoaji wa majiko janja (80L Electric Pressure Cooker) yanayotumia umeme kidogo sana wastani wa ‘units’ 2 kwa saa nzima.

Majiko hayo yameelezwa ni salama na yanajizima yakiivisha ambayo yametolewa kwa shule za sekondari sambamba na kushiriki, pamoja na wadau wengine wa maendeleo, katika Kongamano la Nishati Safi lililofanyika Kizimkazi.

Utoaji wa majiko janja na ushiriki wa Mfuko kwenye Kongamano la Nishati safi ni hatua zinazoonesha dhamira ya NSSF ya kuunga mkono ajenda ya kitaifa ya Nishati Safi ya kupikia, inayolenga kuongeza matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kuboresha afya, kulinda mazingira na kuchochea maendeleo endelevu.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button