Sekta ya maua yapata msukumo mpya Tanzania

DAR ES SALAAM: Mwandaaji wa East Onesho la Africa Flower Expo, Esther Moses Nassari, amesema maonesho hayo yanayotarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza Tanzania, huku yakilenga kukuza na kuimarisha tasnia ya maua pamoja na kuwaunganisha wadau wa ndani na nje ya nchi.
Nassari amesema maonyesho hayo yatafanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Kibiashara cha Ubungo (EACLC) kuanzia Septemba 25 hadi 27, 2026, yakihusisha washiriki kutoka Tanzania na nchi mbalimbali za Afrika Mashariki, zikiwemo Kenya na Uganda, pamoja na Zambia.
Amesema moja ya malengo makubwa ya maonyesho hayo ni kuzindua rasmi Chama cha Wauza Maua Tanzania, ambacho kitakuwa na jukumu la kuwaunganisha wafanyabiashara na wadau wa sekta hiyo ili kubadilishana uzoefu, kutafuta masoko na kuendeleza tasnia ya maua nchini.

Kwa mujibu wa Nassari, uamuzi wa kuwaalika wadau kutoka Uganda na nchi nyingine umetokana na uzoefu alioupata baada ya kushiriki maonyesho ya maua nchini Uganda, ambapo alijifunza namna tasnia hiyo inavyoendeshwa. Amesema pia alibaini kuwa Uganda ina uhitaji wa maua kutoka Tanzania, huku wadau wa nchi hiyo wakionesha nia ya kujifunza na kutafuta wasambazaji kutoka Tanzania.
Nassari amesema sekta ya maua pia inachangia uchumi wa Tanzania kupitia biashara, kodi, ajira na huduma mbalimbali zinazolipwa katika mnyororo wa biashara hiyo. Ameongeza kuwa wafanyabiashara wa maua hulipa tozo na kodi mbalimbali, huku biashara hizo zikiendelea kutoa ajira kwa Watanzania wanaohusika katika shughuli za uzalishaji, usambazaji na uuzaji wa maua.
Amesema East Africa Flower Expo inatarajiwa kuwa jukwaa muhimu kwa wadau wa sekta hiyo kujifunza, kuonesha bidhaa zao, kupata masoko mapya na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Kwa Upande wake Iddi Audi Afisa mawasiliano wa Kituo cha Kimataifa cha Kibiashara cha Ubungo (EACLC)amesema kama Kituo wamejipanga vyema Katika maonesho hayo na itasaidia kukuza Uchumi wa wananchi



