MsingiTek rasmi Manyara kuwezesha wanafunzi kujifunza KKK

Manyara: Zaidi ya wanafunzi 24,000 katika Mkoa wa Manyara wanatarajiwa kunufaika na MsingiTek, programu ya kujifunza kwa kutumia vishikwambi inayolenga kuboresha stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kwa wanafunzi wa Darasa la Kwanza hadi la Tatu.

Programu hiyo inatekelezwa katika shule za msingi wilayani Simanjiro na Kiteto, ambapo awamu ya kwanza ilihusisha shule 50 na kunufaisha zaidi ya wanafunzi 11,000.

Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo kimkoa uliofanyika katika Shule ya Msingi Oloimugi, Wilaya ya Kiteto, Agosti 13, 2026, Katibu Tawala Msaidizi (Elimu) wa Mkoa wa Manyara, Joseph Mabeyo, alisema awamu ya pili, inayohusisha shule nyingine 50, inaendelea na inatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba mwaka huu.

 

Mabeyo alisema programu hiyo tayari imeanza kuonyesha matokeo chanya, huku tathmini zilizofanywa na timu za elimu za mkoa na wilaya zikionyesha kuimarika kwa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu miongoni mwa wanafunzi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Msingi Esukuta wilayani Kiteto, Anna Mgode, alisema matumizi ya vishikwambi hivyo yamepunguza mzigo wa kazi kwa walimu na kurahisisha utoaji wa maarifa ya kusoma, kuandika na kuhesabu kwa wanafunzi, huku pia yakichochea mahudhurio ya wanafunzi shuleni.

Mradi wa MsingiTek unatekelezwa na shirika la Imagine Worldwide kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu– TAMISEMI, Wizara ya Elimu pamoja na wadau wengine katika wilaya 11 za mikoa ya Manyara, Shinyanga, Tabora, Morogoro na Ruvuma.

Mpango huo unaunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha stadi za msingi za kusoma, kuandika na kuhesabu kwa watoto, na unaenda sambamba na mpango mkakati uliozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Januari mwaka huu kwa lengo la kuboresha umahiri wa kusoma, kuandika na kuhesabu kwa watoto wa elimu ya awali na elimu ya msingi ya madarasa ya mwanzo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button