Wawili jela miaka 30 kila mmoja kwa ubakaji

MBEYA; Mahakama ya Wilaya ya Chunya imewahukumu watu wawili kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya ubakaji na ulawiti yaliyotokea katika maeneo tofauti wilayani humo.
Amos Masanja (28), mkazi wa Igangwe, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumlawiti kijana wa kiume mwenye umri wa miaka 20, ambaye jina lake limehifadhiwa.
Hukumu hiyo imetolewa Agosti 13, 2026 na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Chunya,Bruno Bungole.
Mahakama ilielezwa kuwa Masanja alitenda kosa hilo Julai 7, 2026 katika Kijiji cha Igangwe, Kata ya Mtanila,Wilaya ya Chunya, baada ya kumvuta mkono kijana huyo ambaye ana matatizo ya afya ya akili, na kuingia naye katika pagala ambako alifanya kitendo hicho.
Katika tukio lingine, Lusekelo Kajingili (43), mkazi wa kata ya Chalangwa, Wilaya ya Chunya, ambaye ni baba wa kambo wa mwathirika, amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 15, mwanafunzi wa shule ya msingi.
Hukumu hiyo imetolewa Agosti 13, 2026 na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Chunya, Bruno Bungole.
Mahakama ilielezwa kuwa Kajingili alitenda kosa hilo Julai 11, 2026 majira ya saa 4 usiku katika Kijiji cha Chalangwa, baada ya kumvizia mtoto huyo akiwa amelala pamoja na wenzake, kisha kumvua nguo na kumbaka.
Ilielezwa kuwa tukio hilo lilitokea wakati mama mzazi wa mtoto huyo akiwa hayupo nyumbani.



