JWTZ, majeshi EAC kutoa matibabu ya kibingwa bure

DODOMA: JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kwa kushirikiana na majeshi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), linatarajia kutoa huduma za matibabu ya kibingwa bila malipo kwa wananchi.
Kutolewa kwa huduma hizo ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Ushirikiano wa Majeshi ya EAC na Raia yanayoanza Agosti 26 na kufikia kilele Septemba 1, 2026, ambayo pia ni Siku ya JWTZ na kumbukumbu ya miaka 62 tangu kuanzishwa kwa jeshi hilo mwaka 1964.
Akizungumza jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Utawala Jeshini, Brigedia Jenerali Dk Agatha Katua, alisema maadhimisho hayo yatahusisha utoaji wa huduma za afya, misaada ya kijamii pamoja na ukarabati wa miundombinu katika maeneo mbalimbali.
Alisema madaktari bingwa kutoka nchi wanachama wa EAC, zikiwamo Burundi, Kenya, Rwanda, Somalia, Uganda na Tanzania, watashirikiana kutoa huduma katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Arusha na Zanzibar kulingana na mahitaji ya vituo husika.
“Wagonjwa watakaohitaji huduma ambazo hazitaweza kutolewa katika kipindi hicho watapatiwa rufaa kwenda hospitali nyingine kwa kufuata utaratibu wa kawaida.”



