Dk Bashiru afungua kongamano la uvuvi

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Dk Bashiru Ally, amefungua Kongamano la Nne la Kimataifa la Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji (4tFAR4ViBE), huku akisisitiza matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika kuendeleza sekta hizo kwa manufaa ya Taifa.

Kongamano hilo la siku tatu limeanza leo, Agosti 24, 2026, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, likiwakutanisha wanasayansi, watafiti, wataalamu wa vyuo vikuu na wadau wa uvuvi na ukuzaji viumbe maji kutoka nchi 17.

Akifungua kongamano hilo, Dk Bashiru amesema uvuvi ni shughuli inayotegemea sayansi na hivyo inahitaji wataalamu wenye ujuzi, teknolojia za kisasa na ubunifu, ili kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na kuhakikisha wavuvi wadogo wananufaika na shughuli zao.

Amesema matumizi ya tafiti na ushahidi wa kisayansi ni muhimu katika kuboresha usimamizi wa rasilimali za uvuvi na ukuzaji viumbe maji, huku yakisaidia Taifa kutumia fursa zilizopo katika Uchumi wa Buluu kwa njia endelevu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Dk Ismael Kimirei, amesema kongamano hilo litatoa fursa kwa wataalamu kubadilishana taarifa za kisayansi na matokeo ya tafiti yatakayosaidia kuimarisha uendelevu wa sekta ya Uchumi wa Buluu.

Amesema maarifa yatakayopatikana kupitia majadiliano hayo yatachangia katika maendeleo ya sekta ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji, pamoja na kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Katika tukio hilo, Dk Bashiru pia ameshuhudia utiaji saini wa makubaliano ya ujenzi wa meli tatu za Uvuvi wa Bahari Kuu kupitia Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO).

Amesema ujenzi wa meli hizo utaongeza uwezo wa Tanzania kutumia rasilimali za uvuvi katika bahari kuu na kuchangia kuongeza tija ya Bandari ya Uvuvi Kilwa.

“Ujenzi wa meli hizi utaongeza uwezo wetu wa kuvua samaki katika bahari kuu na pia utasaidia kuifanya Bandari ya Uvuvi Kilwa kuwa na tija zaidi,” amesema.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena, amesema Serikali inalenga kuwa na jumla ya meli sita za Uvuvi wa Bahari Kuu, ambapo nne zitakuwa Tanzania Bara chini ya TAFICO na mbili Zanzibar.

Ametoa wito kwa watendaji na wadau wanaohusika na utekelezaji wa mpango huo kuhakikisha ujenzi wa meli hizo unakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.

Naye Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Damas Kamani, amesema ndani ya miezi tisa tangu Dkt. Bashiru aiongoze Wizara, hatua kadhaa zimechukuliwa katika kufufua na kuimarisha TAFICO, ikiwemo mpango wa ujenzi wa meli za Uvuvi wa Bahari Kuu.

Amesema hatua hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuongeza uwezo wa Tanzania katika uvuvi wa bahari kuu na kuhakikisha sekta hiyo inatoa mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa Taifa.

Kongamano la 4tFAR4ViBE linaendelea Dar es Salaam likiwa na ajenda ya kuimarisha ushirikiano wa kisayansi, kubadilishana teknolojia na kukuza tafiti zitakazosaidia maendeleo endelevu ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. Cash earning job to earns more than $700 per day. getting paid weekly more than $3500 or more simply doing easy work online. no special skills required for this job and regular earning from this are just awesome. all you need is 2 hrs a day for this job and earning are awesome. every person can get this by follow details here…

    THIS→→→→ http://Www.Payathome1.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button