Teknolojia, ubia vyatajwa suluhu uhaba wa maji Dar

CHANGAMOTO ya upatikanaji wa maji safi na salama katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam imeendelea kuwaathiri wananchi kiuchumi kutokana na kutumia gharama kubwa ya kupata maji.
Wananchi katika maeneo mbalimbali wanasema kutokuwa na uhakika wa kupata maji kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kumewalazimu kutafuta vyanzo mbadala, hali inayoongeza gharama za maisha na kuathiri shughuli zao za kila siku.
Kwa baadhi yao, maji ya bomba yanaweza kupatikana mara moja kwa wiki, mara moja kwa mwezi au kukosekana kabisa kwa muda mrefu kutokana na hitilafu za miundombinu.
Mkazi wa Shekilango, Zuhura Kangile, anasema kwa kiasi kikubwa wanategemea maji ya DAWASA, lakini upatikanaji wake si wa uhakika.
“Yasipotoka bombani tunalazimika kununua kwa wauza maji ambao wao wanauza ndoo moja Sh1,000, hivyo tunaingia gharama kubwa na huku bado DAWASA watakutumia bili ya maji na hujui maji hayo umetumia lini,” anasema.
Mkazi wa Ubungo, Samweli Swai, anasema katika eneo lao wakati mwingine maji hupatikana mara moja kwa mwezi, hali inayowalazimu wananchi kutafuta njia nyingine za kupata huduma hiyo.
“Kutokana na changamoto iliyopo sasa maji ya DAWASA si ya kutegemea kwetu, inabidi tutafute njia mbadala ya kupata maji,” alisema.
Kwa James Salvatori, mkazi wa Majohe-Pugu, matumizi ya maji ya kisima yamekuwa njia ya kukabiliana na changamoto hiyo.
“Tunatumia maji ya kisima, hatuna shida ya maji kwani yanapatikana muda wote,” alisema.
Hata hivyo, kwa baadhi ya wakazi, hata vyanzo hivyo mbadala havijaondoa kabisa changamoto.
Hatibu Fundi maarufu kama Baba Tuna anasema eneo analoishi limekuwa bila huduma ya maji kwa muda mrefu baada ya bomba kukatika.
“Hatujapata mwezi mmoja sasa bomba limekatika mpaka sasa hawajaja kutengeneza. Tumewaambia waje, wanasema watakuja lakini mpaka sasa hakuna kitu,” anasema.
Anasema hali hiyo imewalazimu kutumia maji ya chumvi huku wakitumia gharama kubwa kununua maji safi.
“Tunatumia maji ya chumvi tu huku, ndiyo njia mbadala na tunatamani kupata maji safi lakini ndiyo hivyo. Tunaingia gharama nyingi kununua maji ambayo si ya chumvi,” anasema.
CAG AIBUA UPOTEVU
Wakati wananchi wakilalamikia upatikanaji wa maji usio wa uhakika, Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeonyesha changamoto nyingine katika sekta hiyo, ikiwamo utekelezaji usioridhisha wa miradi na upotevu mkubwa wa maji.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, DAWASA ilipokea fedha kutoka Serikali zaidi ya bajeti iliyoidhinishwa kwa kiasi cha Sh bilioni 9.69, sawa na asilimia 14, katika mwaka wa fedha 2024/25.
Hata hivyo, pamoja na fedha hizo, mamlaka hiyo haikutekeleza kikamilifu miradi yake ya maendeleo iliyopangwa.
CAG alibaini kuwa kati ya bajeti ya maendeleo ya Sh bilioni 52 iliyoidhinishwa, DAWASA ilitumia Sh bilioni 40.54, sawa na asilimia 77.96, na hivyo kubaki na utekelezaji wa asilimia 22.04 ambao ulielezwa kuwa hauridhishi.

Hali hiyo, kwa mujibu wa ripoti, ilitokana na mambo mbalimbali, ikiwamo mawasiliano duni kati ya Idara ya Ununuzi na Idara ya Ufundi kuhusu mahitaji ya manunuzi, jambo lililoathiri matumizi ya fedha zilizotolewa kwa wakati.
Mbali na utekelezaji wa miradi, CAG alibainisha ongezeko la upotevu wa maji katika baadhi ya miji mikuu.
Dar es Salaam ilionyesha ongezeko kubwa zaidi, ambapo upotevu wa maji uliongezeka kutoka asilimia 41 hadi asilimia 53.
CAG alipendekeza DAWASA iimarishe uratibu na usimamizi ili kuhakikisha fedha zinazotolewa zinatumika kwa wakati kulingana na mipango kazi iliyoidhinishwa.
Pia aliitaka mamlaka hiyo kufanya tathmini ya miundombinu ya maji, kuimarisha mifumo ya kubaini uvujaji, kufanya matengenezo kwa haraka, kudhibiti uunganishaji usio halali na kuwekeza katika teknolojia za kugundua na kupunguza upotevu wa maji.
UBIA WAPEWA KIPAUMBELE
Kwa wataalamu, changamoto hizo zinaonyesha umuhimu wa kutafuta mfumo mpana wa uwekezaji na usimamizi wa huduma za maji unaoweza kuongeza ufanisi na uwajibikaji huku wakisema ushiriki mkubwa wa sekta binafsi kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) unaweza kuwa mwarobaini wa changamoto hiyo.
Msomi na mchambuzi wa sera za kiuchumi, Aurelia Kamuzora, anasema changamoto ya upotevu wa maji na uchakavu wa miundombinu inaweza kupungua iwapo wawekezaji binafsi watahusika kuongeza ufanisi katika matumizi ya rasilimali kwa sababu uwekezaji wao unategemea matokeo, usimamizi mzuri na uwajibikaji.
Anasema wawekezaji hao hawawezi kuvumilia upotevu wa rasilimali unaosababishwa na mabomba yanayovuja, miundombinu chakavu na usimamizi usio na tija.
“Tunapaswa kumanage vizuri. Tukiingiza sekta binafsi, mambo ya kupotea maji hayataonekana hivyo. Uwekezaji wa sekta binafsi umefika wakati mwafaka; tutazalisha maji mengi na tutadhibiti upotevu na kutokana na kuendelea kukua kwa teknolojia kila kitu kitaimarika,” anasema.
Lettice Rutashobya, aliyewahi kuhudumu katika Bodi ya DAWASCO kwa miaka sita, anasema changamoto za ufanisi, ucheleweshaji wa huduma na mianya ya rushwa katika mamlaka za maji zinaweza kupunguzwa kupitia ubia kati ya sekta ya umma na binafsi.

Rutashobya anasema kasi ndogo ya kushughulikia hitilafu za miundombinu, hususan mabomba yanayovuja na kuchelewa kwa huduma za matengenezo, inachangia upotevu wa maji na usumbufu kwa wananchi.
“Mimi kama mtumiaji wa maji nikitembea sehemu nyingi naona kuna upotevu wa maji, mabomba yamepasuka. Kuna sehemu bomba lilipasuka, ilichukua mwaka mmoja na hapo niliripoti DAWASA, hakuna kilichofanyika,” anasema.
Anasema katika baadhi ya maeneo, utekelezaji wa miradi mingine ya miundombinu pia unaweza kuathiri huduma ya maji.
“Unakuta barabara inatengenezwa, bomba linakatwa. Kwa mwezi mmoja hupati huduma ya kuunganishiwa maji na hapo mapato yanapotea,” alisema.
Anaiomba serikali kuharakisha utekelezaji wa mfumo wa PPP katika sekta ya maji ili kuvutia uwekezaji, kuongeza uwajibikaji na kuboresha huduma kwa wananchi.
DAWASA YATOA UFAFANUZI
Akizungumza kuhusu changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi ya maji, Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu wa DAWASA, Christian Christopher, anasema Changamoto za mtiririko wa fedha, upatikanaji wa vifaa, changamoto za kiufundi na ugumu wa ujenzi katika maeneo yenye miundombinu iliyopo zimetajwa kuwa miongoni mwa mambo yanayoweza kuchelewesha utekelezaji wa miradi ya maji nchini.
Anasema utekelezaji wa miradi ya maji jijini una changamoto zake kutokana na mazingira ya ujenzi, ambapo wakati mwingine wakandarasi hulazimika kuchimba mitaro katika maeneo yenye miundombinu mingine kama barabara, mabomba na huduma nyingine zinazotolewa kwa wananchi.
Anasema hali hiyo inahitaji uratibu mkubwa ili ujenzi wa miundombinu mipya usiathiri miundombinu iliyopo na shughuli za kila siku za wananchi, akibainisha kuwa tofauti na maeneo mengine, ujenzi wa miradi ya maji Dar es Salaam unafanyika katika jiji lenye shughuli nyingi na miundombinu iliyokwisha jengwa.
“Changamoto nyingine ni upatikanaji wa vifaa, ambapo wakati mwingine mahitaji ya miradi huwa makubwa kuliko uwezo wa uzalishaji wa ndani, hivyo baadhi ya vifaa hulazimika kuagizwa kutoka nje ya nchi.
Anaongeza “Changamoto za kimataifa za uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa zimewahi kusababisha ucheleweshaji wa upatikanaji wa vifaa vinavyohitajika na wakandarasi.
Anabainisha kuwa mtiririko wa fedha (cash flow) pia unaweza kuathiri kasi ya utekelezaji wa miradi, licha ya Serikali kuendelea kuwekeza katika sekta ya maji ambapo wakati mwingine miradi inakuwa imeidhinishwa kutekelezwa, lakini changamoto ya upatikanaji wa fedha kwa wakati inaweza kusababisha kazi kuchelewa na kuathiri ratiba iliyowekwa.
Anafafanua kuwa Serikali inatekeleza miradi mingi ya maji kwa wakati mmoja katika maeneo mbalimbali nchini, hali inayoongeza mahitaji ya vifaa, wataalamu na rasilimali nyingine.
“Pamoja na changamoto hizo, mamlaka zinaendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi na kutafuta njia za kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinatatuliwa ili miradi ikamilike na wananchi wanufaike.
kuhusu upotevu wa maji anasema katika hatua ya kudhibiti upotevu wa maji DAWASA imeanza kutumia teknolojia za kisasa katika kufuatilia mtiririko wa maji ili kupunguza upotevu wa maji na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa mamlaka hiyo kupunguza utegemezi wa taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu changamoto za huduma, huku ikiweka mifumo itakayowezesha kupata taarifa kwa wakati na kuchukua hatua kwa haraka.
Anasema uwezo wa taasisi hiyo kuitikia taarifa za changamoto umeboreshwa kwa zaidi ya asilimia 50, lakini lengo ni kufikia hatua ambayo changamoto nyingi zitatambuliwa na mamlaka yenyewe kabla ya wananchi kutoa taarifa.
Anasema kwa sasa DAWASA imeanza kutenganisha mifumo ya maji katika maeneo mbalimbali kwa kutumia ‘flow meters’, hatua inayowezesha kujua kiwango cha maji kinachoingia na kutoka katika eneo husika.
“Kwa mfano, mita inaweza kuonyesha kiasi cha maji kilichoingia katika eneo fulani na kiasi kilichotoka, hivyo tofauti kati ya viwango hivyo kusaidia kubaini uwezekano wa kuwepo kwa upotevu wa maji.
“Tunajua kutoka eneo fulani tumeingiza maji kiasi gani na tumebakiza kiasi gani. Kwa mfano, kama maji yaliyoingia ni milioni moja na yanayotoka ni laki mbili, tunajua kuna tofauti ya laki nane ambayo tunapaswa kuifuatilia,” anasema.
Anasema mfumo huo unaiwezesha DAWASA kutambua maeneo yenye upotevu mkubwa na kuelekeza rasilimali katika maeneo hayo badala ya kutegemea taarifa za wananchi pekee.
Aidha, anasema matumizi ya teknolojia yameongezwa kupitia mifumo kama SCADA, inayowezesha wataalamu kufuatilia mita na mwenendo wa mfumo wa maji kupitia vituo vya udhibiti.
“Teknolojia ndiyo kubwa. Tunataka taarifa zetu zije kwa wakati bila kusubiri kuambiwa na wananchi, lakini pia tunataka kujua maji yanapotelea wapi ili tuweze kuchukua hatua,” alisema.
Anasema pamoja na kutumia teknolojia, DAWASA imeanza pia kuwekeza katika matengenezo kinga (preventive maintenance) ili kupunguza hitilafu na mabomba kuharibika, ambazo zinaweza kusababisha upotevu wa maji.
Katika hatua nyingine, anasema DAWASA inahitaji uwekezaji mkubwa katika kuongeza uzalishaji na usambazaji wa maji, hivyo ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha mipango hiyo.
Anasema mamlaka hiyo imeanza kuandaa maandiko yatakayowezesha kupata wawekezaji na washirika binafsi ili kupunguza mzigo wa uwekezaji unaobebwa na Serikali.
“Tunatafuta wadau ili jambo hili liweze kwenda haraka. Kutegemea Serikali pekee kutahitaji uwekezaji mkubwa sana, ndiyo maana tunaingiza wadau ili tuweze kwenda kwa kasi,” anasema.
Anasema pia kuna fursa ya kutumia teknolojia ya desalination katika kuzalisha maji kutoka baharini, ambayo inaweza kuwa sehemu ya suluhisho la kuongeza vyanzo vya maji katika siku zijazo.
Aidha, anasema mpango wa Serikali wa kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji unalenga kuwezesha miradi mikubwa ya maji kutekelezwa kwa kasi, huku Serikali ikielekeza rasilimali zake katika maeneo mengine muhimu kwa wananchi.
Anasema DAWASA itaendelea kutumia teknolojia, kuboresha mifumo ya ndani, kuimarisha matengenezo na kushirikiana na sekta binafsi ili kupunguza upotevu wa maji na kuboresha huduma kwa wananchi.
SERIKALI YAFUNGUA MILANGO
Katika hatua mpya inayolenga kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama nchini, Serikali imetangaza maboresho ya kisera yatakayowezesha sekta binafsi kushiriki zaidi katika uwekezaji, ujenzi na usambazaji wa huduma za maji kupitia mfumo wa PPP.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa sehemu ya mkakati mpana wa kujenga kile kilichoelezwa kama “Gridi ya Taifa ya Maji”, mfumo unaolenga kuunganisha na kusambaza huduma kwa ufanisi zaidi sambamba na matumizi ya teknolojia za kisasa katika uzalishaji, uhifadhi na usimamizi.
Naibu Waziri wa Maji, Kundi Mathew, anasema sekta ya maji ni miongoni mwa sekta zinazohitaji uwekezaji mkubwa na endelevu ambao Serikali pekee haiwezi kuubeba kwa ufanisi bila ushiriki wa sekta binafsi.
Anasema kupitia PPP, Serikali inalenga kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji mijini na vijijini, kupunguza upotevu wa maji, kuongeza matumizi ya mifumo ya kidigitali na kuvutia mitaji pamoja na utaalamu wa kisasa kutoka kwa wawekezaji binafsi.
“Mahitaji ya maji yanaendelea kuongezeka sambamba na ukuaji wa watu, miji na shughuli za kiuchumi. Ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma ya maji kwa uhakika, tunahitaji nguvu ya pamoja kati ya Serikali na sekta binafsi,” anasema.
Maboresho hayo yanatarajiwa pia kufungua fursa za ajira, kuchochea ubunifu wa kiteknolojia na kuongeza ufanisi wa taasisi zinazohusika na huduma za maji.



