Katavi chakula kipo, lakini udumavu unatikisa familia

KATAVI; Wakati Katavi ikizalisha kwa wingi mahindi, mpunga, mihogo, viazi vitamu, maharage, mtama, kunde, karanga, alizeti, ndizi, parachichi, maembe na mboga mbalimbali zinazoweza kutoa virutubisho muhimu kwa afya na ukuaji wa binadamu, mkoa huo bado unakabiliwa na tatizo la udumavu kwa watoto, hali inayodhihirisha kuwa wingi wa chakula pekee haujawa kinga dhidi ya lishe duni.

Mazao hayo yanatoa vyanzo mbalimbali vya nishati, protini, vitamini na madini vinavyohitajika mwilini, lakini uchunguzi umebaini kuwa uwepo wa chakula mashambani hauhakikishi moja kwa moja kwamba watoto wanapata mlo kamili unaokidhi mahitaji yao ya lishe.

Pengo linaonekana katika aina ya vyakula vinavyotumiwa, mchanganyiko wa makundi ya vyakula, idadi ya milo, uwezo wa kaya kumudu vyakula mbalimbali na namna mazao yanayotokana na kilimo na mifugo yanavyotumika katika familia.

Kilimo kwa wingi, lakini Udumavu bado juu

Takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kupitia Utafiti wa Kilimo zinaonyesha nafasi ya kilimo katika maisha ya wakazi wa Katavi.

Kwa mujibu wa takwimu za Utafiti wa Kilimo wa mwaka 2022/23, mkoa huo ulikuwa na kaya 150,583 zilizojihusisha na shughuli za kilimo, sawa na asilimia 1.7 ya kaya zote za kilimo Tanzania Bara. Katika mwaka huo, Katavi ilizalisha tani 186,697 za mahindi, huku wastani wa mavuno ukiwa tani 1.9 kwa hekta.

Hata hivyo, takwimu hizo za uzalishaji zinapaswa kutazamwa tofauti na takwimu za hali ya lishe. Uzalishaji mkubwa wa chakula unaonyesha uwezo wa mkoa kuzalisha mazao, lakini hauwezi peke yake kueleza ubora wa mlo anaopatiwa mtoto.

Ofisa Lishe Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Jackline Kitomari akitoa elimu katika Mkutano wa SALIKI uliofanyika Kijiji cha Itenka Kata ya Itenka.

Kwa mujibu wa Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania wa mwaka 2022 (2022 TDHS-MIS), uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), Wizara za Afya Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na ICF, asilimia 30 ya watoto walio chini ya umri wa  miaka mitano nchini walikuwa na udumavu.

Kwa upande wa mikoa, Iringa ilikuwa na kiwango cha juu zaidi cha udumavu kwa asilimia 56.9, ikifuatiwa na Njombe asilimia 50.4, Rukwa asilimia 49.8, Ruvuma asilimia 35.6, Geita asilimia 38.6, Kagera asilimia 34.3, Simiyu asilimia 33.2, Tabora asilimia 33.1, Mbeya asilimia 31.5 na Katavi asilimia 32.2. Kwa kiwango hicho, Katavi ilikuwa juu ya wastani wa kitaifa kwa asilimia 2.2.

Kwa kulinganisha mikoa ya Tanzania Bara, Katavi ikiwa na asilimia 32.2 iko katika kundi la mikoa kumi yenye viwango vya juu vya udumavu, hivyo, tofauti ya asilimia 2.2 kati ya Katavi na wastani wa kitaifa haiondoi ukubwa wa tatizo, bali inaonyesha kuwa licha ya mkoa kuwa na uzalishaji mkubwa wa chakula, bado kuna changamoto katika kuhakikisha watoto wanapata lishe inayokidhi mahitaji yao.

Chakula kipo, tatizo ni matumizi yake

Uchunguzi uliofanywa katika Mkoa wa Katavi umebaini kuwa changamoto hiyo haiishii katika upatikanaji wa chakula, bali inahusisha pia namna chakula kinavyotumiwa.

Baadhi ya familia zinaweza kuwa na mazao, mifugo, maziwa, mayai, matunda na vyakula vingine lakini watoto wasivitumie kwa kiwango au mchanganyiko unaohitajika kulingana na umri wao.

Afisa Lishe Mkoa wa Katavi, Seleman Hamisi, anasema ulaji wa vyakula mchanganyiko bado ni changamoto, huku matumizi ya vyakula vya asili ya wanyama yakiwa katika kiwango cha chini. Kwa takwimu alizotaja katika mahojiano, ni takribani asilimia 35.7 ya watoto wanaotumia vyakula vya aina hiyo.

. Mganga Mkuu wa Hospitali ya Manispaa ya Mpanda, Dk. Paul Swakala (Kushoto) akiwa na muuguzi wakimuangalia kwa umakini mtoto mwenye umri wa miaka minne aliyeletwa katika hospitali hiyo kwa tatizo la Utapiamlo.

Anasema hali hiyo inaonyesha kuwa upatikanaji wa chakula pekee hauwezi kumaliza tatizo la lishe duni bila kuzingatia aina na mchanganyiko wa vyakula vinavyotumiwa.

Hamisi anaeleza pia kuwa changamoto inaonekana katika idadi ya milo na utofauti wa chakula wanachopewa watoto.

Baadhi ya familia huwaratibia watoto milo kwa kufuata mfumo wa watu wazima bila kuzingatia mahitaji yao ya lishe, huku wengine wakitumia chai au vitafunwa katika muda ambao mtoto angehitaji mlo wenye mchanganyiko wa makundi mbalimbali ya vyakula.

Si utapiamlo pekee: Changamoto ni pana

Kwa mtazamo wa wataalamu wa afya, tatizo la lishe pia lina sura nyingine. Mganga Mkuu wa Hospitali ya Manispaa ya Mpanda, Dk. Paul Swakala, anaeleza kuwa changamoto za lishe katika jamii hazihusiani na utapiamlo pekee, bali pia zinahusisha udumavu, uzito kupita kiasi, unene, upungufu wa damu pamoja na upungufu wa vitamini na madini mbalimbali.

Anasema baadhi ya matatizo hayo yanaweza kuhusishwa na aina ya chakula kinachotumiwa, hasa pale jamii inapokula vyakula vyenye wanga na mafuta kwa wingi bila mchanganyiko wa kutosha wa virutubisho muhimu. Hivyo, changamoto ya lishe haiwezi kupimwa kwa kuangalia tu kama mtu amekula na kushiba, bali pia kile alichokula na kama mlo huo ulikuwa na makundi mbalimbali ya vyakula.

Watoto wafika hospitalini wakiwa wamechelewa

Afisa Lishe Hospitali ya Manispaa ya Mpanda, Neema Kambi, anasema hospitali hiyo hupokea watoto wanaohitaji huduma za utapiamlo kati ya sita hadi saba kwa mwezi, ingawa idadi hubadilika kulingana na wagonjwa wanaofikishwa hospitalini.

Kwa sababu ya eneo la kijiografia la Mpanda, hospitali hiyo pia hupokea wagonjwa kutoka maeneo ya jirani na wilaya zinazozunguka.

Kambi anasema baadhi ya watoto hufikishwa hospitalini wakiwa wamechelewa, huku wengine wakiwa wamevimba au wamekonda sana kutokana na utapiamlo.

Anaeleza kuwa tatizo si lazima liwe kukosekana kabisa kwa chakula nyumbani, kwani mtoto anaweza kupata chakula lakini asipewe chakula kinachokidhi mahitaji yake kwa kuzingatia umri. Familia inaweza kuwa na kuku, ng’ombe, mayai, maziwa na matunda, lakini mtoto asitumie vyakula hivyo kwa kiwango kinachohitajika.

Ushahidi huo unaonyesha tofauti kati ya uzalishaji wa chakula na upatikanaji wa lishe bora. Familia inaweza kulima mahindi na maharage, kufuga kuku au ng’ombe na kuwa na matunda, lakini mtoto bado akakosa protini, mafuta yenye afya, vitamini na madini endapo vyakula hivyo havitaunganishwa katika mlo wake.

Kipato kinavyokwamisha lishe ya familia

Hali hiyo inaonekana pia katika simulizi za baadhi ya familia zilizokutana na changamoto za lishe. Elizabeth Shija Kamsanga, mkazi wa Wilaya ya Tanganyika, anaeleza kuwa familia yake imekuwa ikikabiliwa na changamoto za kipato na uwezo wa kupata mlo wenye mchanganyiko unaohitajika kwa ukuaji wa watoto.

Wakati mwingine, changamoto ya kipato humfanya ashindwe kupata baadhi ya vyakula anavyoelekezwa kutumia licha ya kupata elimu ya lishe kliniki.

Familia nyingine, ya Evalina John, mkazi wa Bujombe katika Wilaya ya Tanganyika, pia ilikumbwa na changamoto hiyo baada ya kilimo cha mahindi na karanga kutompatia unafuu wa kifedha wa muda mrefu. Evalina alikuwa na mtoto wa miezi minne aliyekuwa akinyonya lakini uzito wake haukuongezeka kama ilivyotarajiwa.

Alisema alilima takribani ekari tatu za mahindi na ekari moja ya karanga, lakini sehemu kubwa ya mazao ilitumika katika mahitaji ya familia na hali ya kifedha ikawa ngumu.

Changamoto ya kipato hivyo inaingia katika mnyororo wa lishe kwa namna mbili, kwanza, kaya inaweza kuwa na chakula lakini ikashindwa kununua vyakula vingine vinavyohitajika kukamilisha mlo, na pili, mazao yanayozalishwa yanaweza kutumika kwa mahitaji mengine ya familia na kuacha kiwango kidogo kwa matumizi ya lishe.

Serikali yaweka mikakati ya kubadili hali

Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuf, anasema Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na lishe duni na udumavu, ikiwemo kutoa elimu kwa jamii, kuhamasisha kaya kuwa na bustani za mboga na miti ya matunda pamoja na kufuga kuku na mifugo mingine ili kuongeza upatikanaji wa vyakula vyenye virutubisho.

Jamila anasema changamoto iliyopo ni kubadili namna jamii inavyotazama ulaji wa chakula, kwa sababu kula hakupaswi kuishia katika kujaza tumbo na kushiba, bali mlo unapaswa kuwa na mchanganyiko wa vyakula.

Anaeleza kuwa Serikali pia imeendelea kuhamasisha upatikanaji wa chakula kwa watoto shuleni na kutenga fedha kwa ajili ya masuala yanayohusiana na lishe.

Kitendawili cha Katavi: Chakula kinageukaje kuwa lishe?

Kwa hiyo, kitendawili cha Katavi hakipo katika swali la kama chakula kinazalishwa au la, bali namna chakula hicho kinavyogeuka kuwa lishe kwa mtoto.mahindi, maharage, karanga, mihogo, viazi, mboga, matunda, maziwa, mayai, nyama na vyakula vingine vinapopatikana vinaweza kuwa sehemu ya suluhisho, lakini manufaa yake hutegemea namna vinavyotumika na kuchanganywa katika milo ya familia.

Takwimu za NBS za kilimo zinaonyesha uwezo wa Katavi katika uzalishaji wa chakula, wakati TDHS-MIS 2022 inaonyesha kuwa asilimia 32.2 ya watoto chini ya miaka mitano mkoani humo wana udumavu, ikilinganishwa na asilimia 30 kitaifa.

Wanakijiji cha Itenka Kata ya Itenka wakiwa katika Mkutano wa SALIKI ili wakipata elimu ya Lishe kutoka kwa wataalamu maofisa Lishe.

Pengo hilo la asilimia 2.2 kati ya Katavi na wastani wa kitaifa linaifanya hali ya mkoa huo kuwa swali la msingi la lishe, kwa nini eneo lenye uwezo wa kuzalisha aina mbalimbali za chakula bado lina watoto wanaokabiliwa na udumavu?

Jibu la swali hilo linaenda zaidi ya mashamba na mavuno. Linaelekea katika namna kaya zinavyotumia chakula, kipato cha familia, mchanganyiko wa vyakula, idadi ya milo, elimu ya lishe, malezi ya watoto na imani zinazohusiana na ulaji. Hizo ndizo hoja zinazochambuliwa katika sehemu zinazofuata za uchunguzi huu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button