Zaidi ya wagonjwa 500 wapata huduma ya saratani Mbeya

MBEYA; Zaidi ya wagonjwa 500 wametibiwa magonjwa ya saratani  kwa muda wa miaka mitatu katika hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya.

Akizungumza  wakati wa kupokea msaada wa vifaatiba na dawa kutoka kwa Taasisi ya Jema Foundation, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Saratani Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Dk Tibera Rugambwa amesema hospitali inahudumia mikoa saba ya Mbeya, Iringa, Njombe, Songwe, Ruvuma, Rukwa na Katavi.

Dk Tibera amesema tatizo la saratani ni kubwa katika ukanda huo na ametoa wito kwa wananchi kufika mapema hospitali ili kupata matibabu mapema.

Akitoa msaada huo, Jema Baruani Mkurugenzi wa Jema Foundation amesema amewiwa kutoa msaada huo kwa lengo la kuwatia moyo na matumaini wagonjwa wa saratani kuwa satatani inatibika na kwamba waachane na mila potofu kwenda kwa waganga wa kienyeji wakidhani wamelogwa.

Jema ambaye ni shujaa wa sarani aliyeishi na ugonjwa huo kwa miaka tisa amewaomba wadau wengine kuungana na Taasisi yake ili kuwasaidia wagonjwa wa saratani kwani gharama za vipimo na matibabu yake ni aghali sana.

Akipokea msaada huo Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya,  Dk Awesu Mchepange amemshukuru Jema Baruani kwa msaada alioutoa ambapo ametoa wito kwa wananchi kufika hospitali huduma ambazo awali zilikuwa zikipatikana nje ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini hususani Ocean Road Dar es Salaam.

Amesema kwa sasa wananchi wamepunguziwa gharama kubwa ambazo walikuwa wakizitumia kwa kusafiri umbali mrefu.

Aidha amewataka wadau wengine kuungana ili kusaidia wagonjwa wa saratani kwani gharama za vipimo na dawa ni aghali sana kwa watu wengine wa kipato cha chini hawawezi kuzimudu.

Judith Mwakalinga ni shujaa wa sarani kwa niaba ya wagonjwa wa saratani ameishukuru Taasisi ya Jema Foundation kwa msaada wa dawa na vifaatiba, kwani vitaongeza ari ya utendaji kwa wafanyakazi wa hospitali.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button