Serikali yatoa agizo miradi ya maji Manyara

MANYARA: NAIBU Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Methew, amezitaka Mamlaka za Maji mkoani Manyara kuhakikisha zinakamilisha miradi ya maji iliyofikia hatua za mwisho kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi mipya.

Mhandisi Methew ametoa agizo hilo katika ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Manyara, iliyohitimishwa jana, Oktoba 7, 2026, akisisitiza umuhimu wa kutumia fedha zinazotolewa kukamilisha miradi ambayo imebakiza asilimia chache ili ianze kutoa huduma kwa wananchi.

Amesema azma ya Wizara ya Maji ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa haraka kupitia miundombinu inayokidhi mahitaji yao.

Pia amezitaka mamlaka hizo kuendelea kutafuta vyanzo vipya vya maji, huku akihimiza wananchi ambao ni walaji wa huduma hiyo kuunganisha mabomba ya maji majumbani ili kunufaika na huduma inayotolewa.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Manyara, Mhandisi James Kionaumela, amesema upatikanaji wa maji mkoani humo umefikia asilimia 98 katika maeneo ya mijini na asilimia 84 vijijini.

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Babati, Thobias Abwaro, amemuomba Naibu Waziri wa Maji kuandaa sehemu maalumu ya kuhifadhia maji taka kutokana na kasi ya ukuaji wa Mji wa Babati.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button