Tansfoma nne zasafirishwa kwenda miradi ya Taza

Transfoma nne kubwa zimeanza kusafirishwa kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda katika vituo vya kupoza umeme vya Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa Kilovoti 400 wa Iringa–Kisada–Mbeya–Tunduma–Sumbawanga (TAZA), ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange.
Usafirishaji huo unalenga kuwezesha kukamilika kwa mradi na kuanza kuchaji njia ya umeme kutoka Kituo cha Tagamenda mkoani Iringa kuelekea Sumbawanga kabla ya Novemba 15, 2026.
Meneja wa Mradi wa TAZA, Mhandisi Kelvin Mwasege, amesema timu mbili za usafirishaji zinahusika na zoezi hilo, ambapo timu moja inasafirisha transfoma mbili kuelekea Kituo cha Iganjo mkoani Mbeya na Kituo cha Mkangamo mkoani Songwe, huku transfoma nyingine mbili zikiwa tayari zimefika mkoani Iringa.
“Zoezi hili ni utekelezaji wa maelekezo ya Mkurugenzi wa TANESCO, Lazaro Twange, kuhakikisha kabla ya tarehe 15 Novemba 2026 tunachaji njia yetu ya umeme inayoanzia Kituo cha Tagamenda Iringa kuelekea Sumbawanga,” amesema Mhandisi Mwasege.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Mradi wa TAZA anayesindikiza transfoma hizo katika timu ya pili, Mhandisi Esau Magori, amesema transfoma yenye uwezo wa MVA 250 itawekwa katika Kituo cha Kupoza Umeme cha Iringa, wakati yenye uwezo wa MVA 200 itawekwa katika Kituo cha Kupoza Umeme cha Kisada.
“Hapa tuna transfoma mbili, ambapo yenye MVA 250 tutaifunga kwenye Kituo cha Kupoza Umeme cha Iringa na ya MVA 200 tutaifunga Kituo cha Kupoza Umeme cha Kisada,” amesema.
Amesema kukamilika kwa Mradi wa TAZA kutaiunganisha Rukwa kwenye Gridi ya Taifa na kuweka mazingira ya kuunganisha mifumo ya umeme ya Tanzania na Zambia kwa ajili ya biashara ya umeme.

“Umuhimu wa huu mradi utasaidia kuunganisha Mkoa wa Rukwa kwenye Gridi ya Taifa na zaidi ya yote utakwenda kuiunganisha Tanzania na Zambia katika biashara ya kuuziana umeme,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, alitoa agizo la kukamilisha mradi huo ifikapo Novemba 15, 2026, alipokutana na wakandarasi na wasimamizi wa Mradi wa TAZA mkoani Iringa.



