Wadau wajadili afya ukuaji uchumi, jamii bora

WAKATI Rasimu ya Dira ya Taifa ya 2050 ikibeba nguzo tatu muhimu uchumi imara, jumuishi na shidani kufikia shabaha ya kuondoa umaskini na kufikia pato la mtu Dola 8,000 na taifa Dola bilioni 700, wadau wa maendeleo wamekutana kujadili afya kwa ustawi wa wananchi na taifa.
Pia wadau hao kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania wamekubaliana kuwa suala la uwekezaji katika afya linapaswa kuwa kipaumbele cha afya, afya ya akili na ustawi wa kila mtanzania na hapo ndipo kutakuwa na jamii yenye nguvu katika kufanikisha maono ya kila mmoja na taifa.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Shirika la Women Action Towards Economic Development (Wated) ambapo yameshirikisha wananchi wa mikoa mitano ya Kagera, Lindi, Mtwara, Manyara na Dar es Salaam sambamba na waandishi wa habari.

Akizungumza Februari 24, 2025 katika majadiliano ya pamoja na wadau hao, Mkurugenzi Mwanzilishi wa Shirika la Grace Wellness Service, Grace Kupobota amezungumzia upande wa baadhi ya wanawake kukosa afya njema kwa sababu hiyo ni ngumu kuwa na ustawi.
“Wanawake wengi hawaanzi na wao wenyewe, lakini pia lazima kuwe na umakini na waliowazunguka, ila lazima upate muda wa kutafakari masuala mengi yanayokuzunguka, kwa hiyo anza na mimi,” amesema Grace.
Grace amesema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakijali afya ya kimwili na kusahau kuwa afya ya akili ni muhimu pia katika kumfanya binadamu awaze, kuendesha shughuli zake vizuri, kujali wengine ili kuwa na wanawake, vijana wenye tija kwa ustawi wa taifa.
Akitolea mfano wa afya ya akili inavyoathiri jamii, Ngais Laizer kutoka Shirika la Kinnapa Development Program linalohusika na masuala ya vijana, wanawake mkoani Manyara amesema aliwahi kumchukia mtu hata kumnyima chakula bila sababu na alipojifungua mtoto chuki zikaendelea kwa mtoto na mtu huyo.

“Yule mwanangu alimchukia yule baba kuna siku akamuahidi mwanangu kumpa mbuzi hakumpa basi chuki zikazidi lakini nikaja kujiuliza kwanini ninakuwa hivi nikagundua sababu ni mimi,” amesema Ngais Laizer.
Akiendelea na hoja ya afya ya akili, Grace Kupobota amesema kuwa na afya lazima iwe ya akili, mwili na mazingira na kujiwekeza utaratibu wa kuangalia afya, kujitengenezea utaratibu wa kutafakari mambo mbalimbali na kuyaweka sawa na uhusiano mazuri na jamii ili kuleta urahisi kuelezea changamoto.



