Wazazi washauriwa kuwekeza watoto wa kike

WAZAZI na walezi mkoani Mtwara wameombwa kuwekeza kwa watoto wa kike na wenye mahitaji maalum kwenye fursa mbalimbali za ufundi stadi ili na wao waweze kujitegeme.
Hayo ameyaeleza na Mkuu wa Chuo cha Veta Mkoa wa Mtwara, Theresia Ibrahim kwa niaba ya Mkurugenzi wa Veta Kanda ya Kusini Mashariki wakati wa kuhitimisha mafunzo kwa vijana 69 kutoka mkoani Mtwara wakiwemo wanaume 54 na wanawake 15.
Amesema kumekuwa na wimbi kubwa la wazazi kuona watoto wa kike na wale wenye mahitaji maalum hawawezi kujikita kwenye fani mbalimbali kutokana na maumbile yao jambo ambalo sio sahihi kwani wakiwezeshwa wanaweza na wanauwezo wa kufundishika.

“Katika mafunzo haya wanawake ni wachache pia nimeona kijana mmoja tu mwenye mahitaji maalum wazazi na walezi tuwekeze kwa hawa watoto sio kwamba hawawezi wanaweza wapelekwe wapewe fursa za mafunzo ya ufundi stadi ili waweze kujitegemea”
Mkurugenzi wa Shirika lisiyo la Kiserikali linalojishughulisha na masuala mbalimbali ya Sanaa na Utamaduni la ADEA, Saidi Chilumba, amesema idadi ndogo ya wanafunzi wa kike ni miongoni mwa changamoto waliyokutana nayo.

“Kwa kiasi kikubwa inasababishwa na familia zao pamoja na kutokuwepo kwa wakufunzi wa lugha za alama, nitoe wito kwa vijana wa kike kutokubali kukatatishwa tamaa na wajiamini katika fani zao,”amesema Chilumba
Aidha umuhimu wa fani walizofundishwa vijana hao ni kwamba zitawasaidia kuongeza thamani ya bidhaa watakazoziunda na kuwaingizia kipato.

Baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo akiwemo Asfa Rashidi ameishukuru ADEA kwa kuwapatia mafunzo hayo yatayowapatia fursa kubwa katika maisha yao kwa kuwaongezea ujuzi wataoenda kuutumia katika kazi zao kwa ustadi mkubwa.
Mafunzo hayo ni katika fani mbalimbali ikiwemo uchongaji, uchoraji, seremala na fundi chuma, yaliyoandaliwa na ADEA na kufadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).



