ACT, Chadema wasifu maisha Lowassa

DAR ES SALAAM: MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema wataendelea kuenzi kazi, mawazo na hekima alizowaachia aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa aliyefariki wakati akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jana.
 
Mbowe ameeleza hayo leo kupitia barua ya wazi ya chama hicho kwa umma katika salamu za pole kufuatia taarifa za kifo za Lowassa, aliyewahi kuwa mgombea urais wa CHADEMA mwaka 2015.
 
“Napenda kutoa salamu zangu za dhati, za Pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wapenda demokrasia wote….Mheshimiwa Lowassa alikuwa kiongozi shupavu, mwanasiasa mahiri, mwanaharakati hodari na alikuwa mstari wa mbele katika kupigania mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini mwetu,”
 
“Alikuwa rafiki yangu na mshirika katika safari ya kuleta demokrasia ya kweli Tanzania. Alikuwa mtu mwenye hekima, busara, ujasiri, uzalendo, mtu mwenye huruma, upendo na msamaha kwa wote.

 
“Alikuwa mtu mwenye maono, mipango na mtekelezaji mzuri wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi”.amesema Mbowe.
 
Katika taarifa hiyo Mbowe ameeleza kusikitishwa na kupokea kwa mshtuko taarifa za kifo cha kiongozi huyo ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kuanzia 2005-2008.
 
Chama cha ACT Wazalendo pia kimetoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa
 
Katika taarifa yao ya pole waliyoitoa leo Februari 11, 2024, mwenyekiti wa chama hicho, Juma Duni Haji amemuelezea Lowassa kama kiongozi aliyewatumikia wananchi kwa moyo mkunjufu katika nafasi zake mbalimbali.
 
“Taifa litamkumbuka kwa mchango wake kwenye maendeleo ya nchi yetu, kwa niaba ya ACT Wazalendo na chama na kwa niaba yangu binafsi, natoa pole kwa mama Regina Lowassa na familia nzima ya hayati Lowassa,” imeeleza taarifa hiyo.
 
Aidha, mwenyetiki huyo ametuma salamu za rambirambi kwenda kwa Rais Samia Suluhu sambamba na kutoa pole kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
 
#MwangwiwaUkarimu
#echoesofkindness
#HabarileoUPDATES
/* */