AFRIKA KUSINI; YANGA leo itamenyana na Kaizer Chiefs katika michuano ya Kombe la Toyota mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Free State uliopo Bloem, Afrika Kusini.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu kwani unawakutanisha Yanga dhidi ya kocha wao wa zamani kutoka Tunisia, Nesreddine Nabi ambaye aliwaongoza kutwaa mataji mfululizo kabla ya kuondoka mwaka jana na sasa anawafundisha Amakhosi.
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi alikiri umuhimu wa mechi hiyo akisisitiza malengo yao ni zaidi ya ushindi.
“Mchezo wetu dhidi ya Kaizer Chiefs utakuwa mzuri na wenye ushindani, hasa ikizingatiwa kuwa Chiefs wana kocha mpya,” alisema Gamondi.
“Kila mchezaji atapata nafasi ya kuonyesha uwezo wake. Kwetu sisi, maandalizi yetu yanazidi kuimarika na tunaamini tutacheza vizuri,” aliongeza.
Alisema ziara ya Afrika Kusini imekuwa muhimu kwao wanapojiandaa kwa msimu wa 2024/25 na alisisitiza kuwa mechi hizo ni muhimu kwa ajili ya kujenga timu hasa kipindi chenye wachezaji wapya.
Amakhosi wataingia kwenye mechi hiyo baada ya kutoka Uturuki katika kambi ya zaidi ya wiki tatu kujiandaa na msimu mpya, ambako walicheza mechi kadhaa za kirafiki.
Soma pia: Yanga kuibamiza TS Galaxy leo?
Leo Amakhosi watacheza mbele ya umati wa mashabiki wao kwa mara ya kwanza chini ya uongozi wa Nabi.
Yanga wametoka Mpumalanga baada ya kucheza michezo miwili katika michuano ya Kombe la Mpumalanga na kushinda mmoja dhidi ya Tx Galaxy kwa bao 1-0 na kufungwa na Augsburg ya Ujerumani kwa mabao 2-1.
View this post on Instagram
Huo ni mwendelezo wa kujaribu wachezaji kabla ya msimu mpya kuanza na wameonekana kucheza kitimu, ishara ya kuendelea kuwa tishio msimu ujao huku ikiwa na wachezaji wenye viwango waliosajiliwa ambao ni Prince Dube, Jean Baleke, Clatous Chama na wengine.
Baada ya mchezo dhidi ya Kaizer Chiefs wanatarajia kurejea nchini Julai 30 kwa maandalizi ya Kilele cha Wiki ya Mwananchi, Agosti 4, mwaka huu ambapo wanatajwa kucheza na Waydad Casablanca.