KKKT yazindua jukwaa la mafunzo, kitabu kidijitali

DAR ES SALAAM: Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limezindua tovuti ya mafunzo ya kidijitali, KKKT Digital, itakayotoa mafundisho ya Kikristo na ujasiriamali, sambamba na uzinduzi wa kitabu kipya cha Mchungaji Dk Allen Mbiso, Yesu Kristo Mponyaji, kitakachopatikana kupitia jukwaa hilo la kidijitali.

Tovuti hiyo imeundwa kuwezesha watumiaji kupata mafundisho mbalimbali ya Kikristo, mahubiri, nyenzo za uanafunzi pamoja na mafunzo ya ujasiriamali, hivyo kuwapa fursa ya kujifunza popote walipo kupitia teknolojia ya kidijitali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Mchungaji Dk Mbiso alisema ongezeko la matumizi ya majukwaa ya kidijitali limefungua fursa mpya ya kueneza Injili sambamba na kuwajengea watu maarifa ya vitendo yatakayowawezesha kuboresha maisha yao kiuchumi.

Alisema kitabu hicho kinalenga kuwasaidia watu kuelewa nguvu ya uponyaji wa Mungu na kuimarisha juhudi za uinjilisti nchini.

Kwa mujibu wa Mchungaji huyo, kitabu hicho ni chanzo cha hamasa na tafakari kitakachowasaidia wasomaji kupata uelewa mpana zaidi kuhusu kazi ya Mungu, uwezo wake wa kubadilisha maisha ya watu pamoja na athari za neema, uponyaji na uongozi wake katika safari ya mwanadamu.

“Leo watu wengi hutumia muda wao mwingi kwenye majukwaa ya mtandaoni. Tunataka maeneo hayo yawe sehemu ambazo watu watakua kiroho na wakati huo huo wapate maarifa yatakayowawezesha kiuchumi,” alisema.

Akifafanua zaidi kuhusu tovuti hiyo, alisema *KKKT Digital* itapatikana kwa watumiaji ndani na nje ya Tanzania, ikiwawezesha kusoma mafundisho ya Biblia na kozi za ujasiriamali kwa wakati unaowafaa.

Katika hafla hiyo, Mchungaji Dk Mbiso pia alizindua rasmi kitabu chake Yesu Kristo Mponyaji, akisema mapato yatokanayo na mauzo yake yatatumika kuimarisha shughuli za uinjilisti nchini.

Alisema fedha hizo zitaelekezwa katika ununuzi wa vifaa vya uinjilisti, ikiwemo magitaa, vipaza sauti, jenereta na vifaa vingine vitakavyosaidia kuifikisha Injili katika jamii mbalimbali.

Alieleza kuwa kitabu hicho kinakusudia kuwasaidia wasomaji kumwelewa Yesu Kristo si tu kama Mwokozi bali pia kama Mponyaji.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini na Mratibu wa KKKT Digital, Geoffrey Kilimba, alisema jukwaa hilo litapanua upatikanaji wa mafundisho ya Kikristo na ujuzi wa vitendo kwa kuwawezesha watu kujifunza wakiwa majumbani, sehemu za kazi au popote penye huduma ya intaneti.

Alisema matumizi ya teknolojia ya kidijitali yataisaidia Kanisa kuwafikia watu wengi zaidi na kuendana na mabadiliko ya namna jamii inavyopata taarifa na elimu katika zama za sasa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button