Mpango atoa agizo uzalishaji simu janja
MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ameziagiza Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji) kuweka mkazo katika kutafuta wawekezaji wanaoweza kuzalisha simu janja nchini.
Pia ameiagiza Wizara ya Fedha kuangalia upya kodi ili wananchi wapate huduma ya simu janja kwa unafuu. Akizungumza wakati wa kuzindua jengo la ofisi za Makao Makuu ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano, Dk Mpango alisema anatambua kuwapo kwa changamoto ya kutosambaa kwa simu janja nchini.
“Nimekusikia vizuri kuhusu changamoto ya kutosambaa kwa simu janja, hivyo niagize wizara inayosimamia masuala ya uwekezaji iweke mkazo katika kutafuta wawekezaji wanaoweza kuzalisha simu janja hapa nchini na kwa Waziri wa Fedha hebu mziangalie tena hizi kodi ili wananchi wetu waweze kupata huduma ya simu janja,” alisema.
Aidha, ameitaka UCSAF kuendelea kusimamia kwa karibu ujenzi wa minara ya mawasiliano unaoendelea na kuhakikisha vijiji ambavyo havina huduma za uhakika za mawasiliano ya simu vinapata mawasiliano.
“Wananchi wetu wanayo haki ya kupata mawasiliano ya uhakika wakati wote ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi, hususani katika kipindi hiki ambapo huduma nyingi zinawezeshwa na huduma za mawasiliano,” alieleza.
Ameiagiza wizara kushirikiana na wadau kuona uwezekano wa kuiongezea UCSAF uwezo, ikiwamo fedha na rasilimali nyingine ili kuiwezesha kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo yasiyo na huduma ya televisheni au redio za nchini.
“Pia UCSAF iangalie uwezekano wa kuwezesha matangazo ya televisheni na redio kuwafikia wananchi kwa njia ya mtandao na kuwa sekta binafsi inayo nafasi ya kushirikiana na UCSAF katika utoaji wa huduma hizo,” alieleza.
Aidha, ameitaka UCSAF iendelee kutekeleza miradi ya kuongeza uwezo wa minara kutoka teknolojia ya 2G kwenda 3G na 4G ili ikiwezekana nchi ihame kabisa kutoka kwenye teknolojia hiyo na kuhakikisha huduma na
mawasiliano na intaneti zinapatikana kwa wananchi wote mijini na vijijini.
“Tunapoadhimisha miaka 60 ya Muungano wetu ni wakati sasa tujitazame namna nzuri ya kutumia muda wetu, panapokuwapo na shughuli kama hizi basi twende kwa wakati hata wale wanaowahi nao wanashughuli nyingine za kufanya,” alisema.
Dk Mpango ametumia fursa hiyo kuzikumbusha taasisi za serikali ambazo hazijahamia Dodoma kufanya hivyo na kwa zile ambazo tayari zimehamia Dodoma, lakini hazina majengo yake kuhakikisha zinaanza na kukamilisha ujenzi wa ofisi ili kuepuka kutumia fedha nyingi za serikali kulipa kodi ya pango kwa muda mrefu. Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alimpongeza Makamu wa Rais.
“Leo (jana) kuna jambo umetufanyia. Alituambia saa tatu kamili nitakuwepo hapo, tumezoea wakiwambia saa tano wanakuja saa sita na viongozi wanakuja saa saba, lakini Mheshimiwa Makamu wa Rais ulisema saa tatu kamili, saa tatu kasoro tumekupokea asante sana,” alisema Nape.